Mkurugenzi TAMWA ZNZ Ataka Vijana, Wanawake Kujiamini Kugombea Nafasi Za Uongozi
Mkurugenzi TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa akizungumza wakati wa mafunzo ya uongozi kwa Vijana wa kike.
MKURUGENZI wa Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Dkt. Mzuri Issa, amewashauri wanawake
na Vijana kujiamini na kuondosha woga wakati wa kugombea nafasi za Uongozi ili
kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Dkt. Mzuri ameyasema hayo akifungua mafunzo ya
siku mbili ya uongozi kwa vijana wa kike, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa
kuungana pamoja na kuleta ushawishi katika maendeleo ya agenda mbalimbali za
kitaifa.
Amesema kwa sasa dunia imetambua umuhimu wa
mwanamke na imeamini kwamba mwanamke ni Kiongozi kutokana na maendelo tofauti
yaliyoletwa na viongozi wanawake duniani.
“Mwanamke ni kiongozi bora, na nyinyi vijana ndio
tunawategemea muwe na maono ya mbali katika kuleta uongozi ulio imara na
kuibeba nafasi ya mwanamke katika uongozi, mwanamke anaweza kuwa mama, mke,
mfanyakazi na kiongozi na wakati huohuo na akaweza kutekeleza majukumu yote
hayo na akafanya vizuri katika kila sekta”, Dkt. Mzuri Issa , Mkurugenzi TAMWA
ZNZ.
Akitoa mafunzo hayo kwa vijana wa kike 15,
Mkufunzi wa masuala ya Uongozi, Imelda Lulu Urrio amesema lengo la mafunzo hayo
ni kuwajengea uwezo kujitambua na kutambua nafasi zao ili kufikia ndoto zao
katika harakati za Uongozi.
“Nafasi ya wanawake kwa sasa inazidi kuongezeka
kwa sababu kuna ukuwaji wa Elimu kwa jamii na hata watoto wa kike wenyewe
wameanza kujitambua na kujielewa, tumeona baadhi ya jamii inavyowajenga watoto
wa kike kujitambua na kupelekea ongezeko kubwa la viongozi wanawake”, alisema
mkufunzi huyo.
Nae Maryam Ame, mratibu wa mradi wa kuwawezesha
wanawake kushika nafasi za Uongozi (SWIL) unaotekelezwa na TAMWA ZNZ kwa
kushirikiana na Ubalozi wa Norway amesema mda mrefu imeonekana wanawake
wameachwa nyuma katika ngazi za maamuzi hivyo kwa sasa wanawake watumie fursa
na haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa ili kufikia dhamira ya 50/50
katika masuala ya uongozi.
Aidha washiriki wa mafunzo hayo wamesema
wamefarijika kupata mafunzo hayo kwani yanawajenga kuwa viongozi bora na
kuahidi kuwatakuwa mabalozi wazuri kwa wanawake na kupambana kugombania nafasi
za ngazi za juu ili kuondosha mfumo dume uliotawala katika jamii.
“Matarajio yangu baada ya mafunzo haya ni kuwa
Kiongozi mwenye kujiamini, na nitapambana kuwa kiongozi wa ngazi za juu zaidi
katika chuo changu,” alieleza Hudhaimat Haji Juma, mwanafunzi wa Shahada ya
Pili ya Uhasibu katika Chuo Kikuu cha Taifa, (SUZA).
Mafunzo hayo yameendeshwa ikiwa ni mwendelezo wa
utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL),
unaotekelezwa kwa pamoja na TAMWA ZNZ, PEGAO NA ZAFELA kwa mashirikiano na
Ubalozi wa Norway.
Post a Comment