SHAKA AWEKA WAZI SERIKALI INAYOONGOZWA NA RAIS SAMIA INAVYOFUNGUA MAENDELEO
Na
Mwandishi Wetu, Iringa
MKUU wa Wilaya Kilosa mkoani Morogoro Shaka Hamdu Shaka,
amesema kazi kubwa inayofanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan
inaongeza kasi ya maendeleo na kuihakikishia nchi kupaa kiuchumi.
Amesema ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kiuchumi
zikiwemo barabara, Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) na ununuzi wa ndege
kubwa ni miongoni mwa hatua za uhakika katika kuleta maendeleo endelevu.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa kongamano la uwekezaji
lilofanyika ukumbi wa Royal Palm mkoani Iringa Shaka aliyemwakilisha Mkuu
wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema pia mkakati wa usambazaji umeme
unaotekelezwa na Serikali utafanikisha vijiji vyote nchini kupata umeme ifikapo
Juni 2024.
Amesema nishati ya umeme ni muhimu kwa maendeleo hususan
katika kuvutia uwekezaji mkubwa na kwamba kazi kubwa inayofanywa na Serikali
katika kufanikisha maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla inapaswa kuungwa
mkono na kila mmoja wetu.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 za Afrika zinazokua kwa
kasi kiuchumi. Kwa miaka 10 iliyopita uchumi wa nchi ulikua kwa wastani wa
asilimia saba. Julai mwaka 2020, Benki ya Dunia (WB) iliipaisha Tanzania kuwa
nchi ya uchumi wa kipato cha mwanzo cha kati.
“Mafanikio haya yanachagizwa na amani, utulivu wa kisiasa
na kiuchumi pamoja na sera nzuri zinazotabirika. Kwa sasa uchumi wetu unakua
kwa asilimia 5.2 ukiwa unainuka kutoka katika athari za Uviko-19 ni dhahiri
kuwa tunakwenda vyema,” amesema Shaka.
Ameongeza Tanzania imeendelea kutoa fursa nyingi
katika sekta zote na kwamba serikali inaweka kipaumbele zaidi katika maeneo
muhimu kikiwemo kilimo, madini, utalii, ufugaji, uvuvi, gesi asilia, viwanda na
Teknolojia ya Hbari na Mawasiliano (TEHAMA).
“Serikali imedhamiria na kujitoa kuifungua nchi katika
uchumi wa dunia kutokana na maboresho kwa sekta ya biashara na uwekezaji
kupitia uendelezaji wa miundombinu mikubwa.
“Hatua hizo zinalenga kuharakisha mtiririko mzuri wa
wawekezaji wa moja kwa moja wa nje (Foreign Direct Investments - FDI) na
uwekezaji wa moja kwa moja wa ndani (Direct Domestic Investments - DDI) kwa
ustawi wa jamii na uchumi wa Watanzania,” amesema.
Akieleza zaidi amesema Serikali imefanya mageuzi makubwa
ya kisheria, kikanuni, kikodi na kiforodha, mifumo na taasisi, utendaji kazi na
matumizi ya TEHAMA pamoja na kuondoa vikwazo vinavyozuia ukuaji wa
biashara."Lengo ni kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo bora ya
uwekezaji Afrika."
Akizungumzia ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la
Nyerere lenye thamani ya dola za Marekani bilioni tatu litakapokamilika
litakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 2,115, amesema litakuwa
msaada mkubwa na kutoa msukumo katika ukuaji wa uchumi.
Post a Comment