SAMATTA AWEKA HISTORIA MBELE YA WAYNE ROONEY, APIGA BONGE LA BAO

Mtanzania Mbwana Samatta ameandika historia ya kuwa Mtanzania aliyeweza kufunga bao dhidi ya timu ya Everton ambayo inashiriki Ligi Kuu ya England baada ya kufanya hivyo katika mchezo wa kirafiki akiwa ndani ya jezi ya KRC Genk.
Samatta ambaye amekabidhiwa jezi namba tisa hivi karibuni katika kikosi hicho, amefanikiwa kuifungia timu yake hiyo bao katika dakika ya 55 katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Everton ambao walikuwa na staa wao, Wayne Rooney.
Bao la Samatta lilipatikana baada ya kupigwa pasi zaidi ya saba kuanzia kwa kipa wa Genk hadi mpira ulipomfikia Samatta ambaye alimalizia kwa kupiga shuti kali. Mchezo huo uliochezwa Jumamosi hii  nchini Ubelgiji ni maalum kwa ajili ya kujiandaa na msimu wa 2017/18 kwa timu zote mbili.
Bao la Everton lilifungwa na Rooney katika dakika ya 45.
Samatta amekuwa na mwendelezo mzuri katika mechi za maandalizi ambapo wiki iliyopita pia alifunga bao moja katika sare ya mabao 3-3 ya timu yake dhidi ya Ajax ya Uholanzi.

No comments

Powered by Blogger.