Walimu wanne watumbuliwa kwa tuhuma za kufanya mapenzi na wanafunzi

Walimu wanne wa shule ya sekondari Kitumbeine wilayani Longido,  Arusha, wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi baada ya kutuhumiwa kujihusisha na mapenzi na wanafunzi wao.
Akisoma risala kwa mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye yupo wilayani humo kwa ziara ya siku tano ya kukagua maendeleo na changamoto, Mkuu wa wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alisema hivi sasa uchunguzi unafanyika, kubaini jinsi walimu hao walivyojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao.
Chongolo alisema uchunguzi utakapokamilika na ikithibitika, watachukuliwa hatua za kinidhamu. 
Alisema pia kuwa kuna changamoto ya mimba ya utotoni, ambazo baadhi ya wazazi na walezi wao wamekuwa wakiwaozesha kutokana na mila.
Aidha Chongolo alisema serikali inafuatilia wazazi wenye tabia hiyo ya kuwaozesha watoto wenye umri mdogo kwani tatizo hilo lipo kwa asilimia 13 katika jamii ya wafugaji.
“Tupo kwenye uchunguzi ili kubaini kama kweli walimu hao wamehusika na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao au lah na endapo ikithibitika kuhusu hilo hatua kali za kinidhamu zinafanyika,” alisema bila kuwataja majina wahusika hao.
Hata hivyo, alisema mimba za utotoni zimepungua ingawa bado kuna changamoto ya wasichana kuozeshwa kwenye umri mdogo na wazazi wao.
BY: EMMY MWAIPOPO

No comments

Powered by Blogger.