Lema Aendelea Kugoma Kula Akiwa Mahabusu, Kufikishwa Mahakamani Leo
MBUNGE wa Arusha Mjini,
Godbless Lema (Chadema), ameendelea kugoma kula kwa siku ya tatu
mfululizo tangu alipokamatwa Oktoba 26 mwaka huu, nyumbani kwake mjini
hapa, akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi.
Lema alikamatwa siku hiyo saa 12
alfajiri akiwa nyumbani kwake, Njiro, na hadi sasa anashikiliwa katika
mahabusu ya kituo kikuu cha polisi mjini Arusha.
Kutokana na kuendelea kugoma kula,
Wakili wake, John Mallya amesema leo saa sita mchana atakwenda Mahakama
Kuu, Kanda ya Arusha kufungua kesi ya kutaka mteja wake afikishwe
mahakamani.
Malya jana alisema katika kesi hiyo
atashirikiana na Chadema kuwashtaki mwendesha mashitaka mkuu wa Serikali
na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai, Mkoa wa Arusha.
Tangu mbunge huyo akamatwe amegoma kula kwa kile anachodai kupinga udhalilishwaji aliofanyiwa na polisi wakati wa kukamatwa.
Pia, Lema anasema alinyanyaswa mbele ya watoto wake nyumbani kwake huku wakijua yeye ni kiongozi na amechaguliwa na wananchi.
Neema, mkewe Lema,jana alithibitisha kwamba mumewe amegoma kula.
“Anaendelea kugoma kula mpaka sasa kwa sababu hata sasa nimetoka polisi asubuhi kumpelekea chakula, lakini amekataa kula.
“Lakini nilipouliza pale polisi kuwa wanampeleka lini mahakamani, nilijibiwa wanaendelea kumhoji,”alisema Neema.
Juzi, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa
Arusha, Charles Mkumbo, alithibitisha kukamatwa kwa Lema na kueleza kuwa
alihojiwa dhidi ya matamshi ya uchochezi na kuwa atafikishwa mahakamani
baada ya kukamilika uchunguzi.
Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, Lema
anatuhumiwa kuwachochea wakazi wa Arusha kuandamana Septemba mosi, mwaka
huu kuhamasisha kile kinachoitwa Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania
(Ukuta).
Aidha Kamanda Mkumbo ameongeza kuwa ikithibitika Mbunge Lema amegoma
kula kwa sababu zisizo na msingi, atafunguliwa shitaka la kujaribu
kujiua. Amesema anachokifanya mbunge huyo kugoma kula chakula ni kosa
la jinai sawa na kujinyonga au kujiua kwa sumu.
Post a Comment