Mastaa Hawa Wamekopi na Kupesti Hadi Nywele?
Andrew Carlos
MASTAA wa Bongo bwana! Baada ya
kukopi na kupesti staili ya kuimba na biti zao nyingi kufanana na za
Sauz na Nigeria ni kama wamehamia kwenye staili mpya ya usukwaji nywele
inayotumika hasa kwa mastaa nchini Marekani.
Ukiwaangalia muonekano wa vichwa vyao,
baadhi ya mastaa hawa wakiongozwa na Jux, Romy Jones, Harmonize na
wengine kibao utagundua kuna kitu wamekopi na kupesti kutoka kwa mastaa
wa mbele ambao ni Chris Brown, Post Malone, The Game, Omario na wengineo
Inaitwaje?
Staili hii iliyotokea kujizolea umaarufu
mkubwa kwa mastaa mbalimbali hususan wa muziki inajulikana kama Dutch
Braid japokuwa chimbuko hasa la staili hii lilikuwa likijulikana kama
French Braid.
Staili hii ipoje?
Usukwaji wake huwa wa nywele kuanzia njia mbili kubwa kisha kwa nyuma inafungwa ama kuachiwa mikia.
Mastaa wengi wa kike kama Kim
Kardashian, Karrueche na wengineo wanapenda kusuka njia mbili ndefu za
kuacha mkia ukining’inia na kwa upande wa mastaa wa kiume, pande zote za
pembeni hunyoa na katikati husuka njia mbili ama tatu kisha huzifunga
kwa nyuma.
Post Malone
Staa huyu wa muziki nchini Marekani
ambaye pia ni rafiki mkubwa wa Justin Bieber, amekuwa akibadili staili
ya nywele zake mara kwa mara.
Ukicheki baadhi ya video zake za hivi
karibuni alizofanya na wakali kama Young Thug, 50 Cent na Kanye West
kichwani kwake utamuona katika muonekano wa Ki-dutch.
The Game
Mei mwaka huu, kupitia ukurasa wake wa
Instagram, kwa mara ya kwanza rapper The Game aliitambulisha staili hii
ya Duth kwa mashabiki wake.
Rapa huyu kutoka Los Angeles, Marekani
aliiweka picha mtandaoni akiwa saluni katika matengenezo ya staili ya
Dutch na baada ya hapo alipewa shavu la kutosha kutoka kwa mashabiki.
Chris Brown
Mkali huyu wa R&B kwa miaka mingi
amekuwa hatabiriki katika staili zake za nywele lakini baada ya staili
hii kuteka mastaa wengi naye amekuwa miongoni mwao.
Chris ambaye ni baba wa mtoto mmoja,
Royalty amekuwa akitupia picha zake mitandaoni zikimuonesha katika
muonekano wa Ki-dutch lakini kwa staili mbalimbali.
Jux
Kuonesha kuwa mastaa wa Bongo hawapitwi
na kitu katika kukopi na kupesti, staa wa Ngoma ya Wivu, Jux amekuwa
miongoni mwa mastaa Bongo waliotekwa na staili hii.
Jux ameonekana kula sahani moja na Chris
Brown. Mara ya kwanza Chris alitengeneza staili hii ya Dutch kizamani
kwa kuning’iniza nywele mbili mbele na nyuma kubana, Jux alipoona
akakopi na kupesti.
Chris akabadili staili hiyo na kunyoa za
pembeni, nyuma akizibana. Jux kuona hivyo naye akaiga tena ambayo ndiyo
anayo hadi sasa.
Harmonize
Staa huyu anayebamba na Ngoma ya
Matatizo, baada ya kuongeza michoro kadhaa mwilini mwake (tattoo),
ameamua kubadili na staili ya nywele.
Alichokifanya kichwani kwake, amejaribu
naye kukopi na kupesti staili ya Dutch ambapo kwa sasa amekuwa akitupia
picha nyingi na vipande vya video akiinamisha kichwa ili mashabiki wake
waione staili hiyo mpya ya nywele.
Romy Jones
Hivi karibuni, binamu na DJ wa staa wa
muziki wa Bongo Fleva, Diamond, Romy Jones katika kusherehekea siku yake
ya kuzaliwa iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Next Door, jijini Dar
aliingia na sapraizi kichwani kwake akiwa katika muonekano wa Ki-dutch.
Kama ulivyo muonekano wa nywele kwa sasa
wa Omario, Chris Brown na The Game kwa Rommy hakuna tofauti yoyote
kwani naye amekopi na kupesti tu.
Post a Comment