AVEVA AACHIWA KWA DHAMANA, TAKUKURU YAFUNGUKA SABABU ZA KUMSHIKILIA, YASIMULIA FEDHA ZILIZOHAMISHWA KWENDA HONG KONG

Huku Rais wa Simba, Evans Aveva akiwa ameachiwa kwa dhamana, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) imesema ilimshikilia kwa kuwa fedha dola 300,000 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Simba katika benki moja, kwenda kwenye akaunti na benki nyingine.

Fedha hizo ni zile za malipo ya mwanasoka Emmanuel Okwi aliyeuzwa dola 319,212 lakini fedha hizo hazikulipwa mapema baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kufanya haraka katika mauzo hali iliyofanya uongozi wa Simba ulioingia madarakani kuanza kuhaha kupambana na Etoile hadi kufikia Fifa ili walipwe.
Mkuu wa Uchunguzi wa Sekta ya Umma ya Takukuru, LEonard Mtalai amesema akaunti hiyo iliyohamishiwa dola 300,000 ni ya Aveva na baada ya hapo, dola 62,000 zilihamishwa kwenda Hong Kong na sasa Takukuru inashirikiana na wenzao wa nchini humo ili kujua kilichonunuliwa kupitia fedha hizo.

Taarifa nyingine, zinaeleza fedha hizo dola 62,000 zilitumika kununua nyasi bandia ambazo tayari zimetua nchini kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mazoezi eneo la Bunju na ujenzi umeanza.

Ofisa huyo wa Takukuru, amethibitisha kuhojiwa kwa watu kadhaa pamoja na Aveva na kusema bado wanaendelea na uchunguzi.

“Tutajitahidi kadiri ya uwezo wetu kuendelea na uchunguzi ili ukikamilika, kama tutagundua kuna matatizo basi mara moja sheria itafuata mkondo wake,” alisema.

Awali, alieleza waliamua kuanza uchunguzi baada ya kupata taarifa za kiintelejensia kwamba kuna fedha nyingi zilihamishwa kutoka kwenye akaunti moja kutoka katika benki moja, kwenda akaunti nyingine katika benki tofauti.


“Hii ilitufanya mara moja kuanza uchunguzi,” alisisitiza Mtalai.

No comments

Powered by Blogger.