Askofu Gwajima Aibuka.......Azungumzia Sakata lake Kanisani, Msaidizi wake Akanusha Kanisa Hilo Kufungiwa

KIONGOZI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, amefunguka kwa kuelezea safari yake aliyoifanya nje ya nchi hivi karibuni, baada ya taarifa mbalimbali kudai kuwa alilikimbia Jeshi la Polisi.


Akiongoza ibada kanisani kwake, Ubungo, jijini Dar es Salaam jana, Askofu Gwajima alisema aliondoka nchini kwenda Japan Juni 15, mwaka huu, kwa ndege ya Emirates.


Akitoa mahubiri katika ibada jana, Gwajima alisema alifika mjini Osaka Juni 16 na kuanza mkutano wa kuhubiri injili na siku zilizofuata alikwenda katika miji mbalimbali.


Askofu Gwajima ambaye aliingia kanisani hapo saa 5:00 asubuhi na kuanza kuhubiri dakika 15 baadaye, asubuhi alitumia muda wa saa tatu hadi saa 8:20 kumaliza mahubiri yake.


Baada ya kuanza kuhubiri, alielezea safari hiyo kwa kutaja miji aliyekwenda ikiwamo Nagoya alikohubiri kwa siku mbili, Karuizawa, Ibaraki, Hiloshima na Yanakochi.


“Safari yangu ilikuwa ya mafanikio sana. Tulisafiri salama na kuzunguka miji mbalimbali na tulirudi Jumatatu ya wiki iliyopita,” alisema Askofu Gwajima.


Kadhalika, katika mahubiri hayo, Gwajima aliwakumbusha waumini wa kanisa hilo kuhusu kuhama kwa kanisa hilo, kwa kuwatajia siku ya mwisho ya kumalizia michango kwa ajili ya ujenzi wa kanisa jipya kuwa ni Julai 30, bila ya kutaja sehemu ambayo kanisa hilo litahamia.


Hata hivyo, Askofu Gwajima wakati wote wa mahubiri, hakuzungumzia suala la kuhojiwa kwake na Jeshi la Polisi.


Wakati huo huo, mwandishi alizungumza na Msaidizi wa Askofu Gwajima, Yekonia Bihagaze, kuhusu tetesi za kufungiwa kwa kanisa hilo na kusema taarifa hizo si za kweli bali ni maneno ya mitaani.


“Hayo maneno si ya kweli. Si umeona ibada imeendelea kama kawaida na Askofu amehubiri? Maneno ya mtaani usiyalete kanisani,” alisema Bihagaze.


Julai 12, mwaka huu, Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) kilimkamata Askofu Gwajima wakati akitokea Japan kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.


Baada ya kukamatwa, alipelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa, akidaiwa alitoa maneno ya uchochezi mwezi uliopita.


Jeshi la Polisi lilikuwa likimtafuta Askofu Gwajima baada ya kusambazwa mkanda kwenye mitandao ya kijamii unaodhaniwa una sauti yake.


Katika mkanda huo, Gwajima anapendekeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete afikishwe mahakamani kwa yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake, ambayo kwa sasa Rais Magufuli anayashughulika kwa staili ya utumbuaji majipu.


Pia Gwajima alisikika akimshauri Rais John Magufuli, kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) iwapo watakataa kumkabidhi uenyekiti na kwamba apeleke muswada bungeni, kuondoa kinga ili rais ashtakiwe kwa makosa aliyoyafanya akiwa madarakani.


Tangu kusambaa kwa mkanda huo, Jeshi la Polisi lilikuwa likipiga kambi katika moja ya nyumba za Askofu Gwajima, iliyoko Mbezi Salasala jijini Dar es Salaam.


Pamoja na kupiga kambi, jeshi hilo halikufanikiwa kumkamata na baadaye ilielezwa kuwa amekwenda nje ya nchi kuhubiri.

No comments

Powered by Blogger.