Serikali Yapongezwa kwa Kuwaleta Pamoja wadau wa Mazingira na Wazalishaji Mifuko ya Plastiki

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akifungua Kikao cha Wazi cha kupokea maoni ya wadau kuhusu dhamira ya Serikali kupiga marufuku uzalishaji,uuzaji,usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki leo Jijini Dar es Salaam.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustine Kamuzora akiongea wakati wa ufunguzi wa Kikao hicho leo Jijini Dar es Salaam.Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba.
 Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Richard Muyungi akiongea wakati wa Kikao hicho mapema leo.
 Mwenyekiti wa Umoja wa wazalishaji wa mifuko isiyo na athari kwa mazingira Bw. Jumanne Mgude akionesha mfuko unaozalishwa hapa nchini usio na athari kwa mazingira wakati wa Kongamano hilo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Wande Printing and Packaging (T) Ltd Bw. Joseph Wasonga akitoa maoni ya wamiliki wa Viwanda vya Kuzalisha mifuko ya plastiki hapa nchini wakati wa kikao hicho. 
 Katibu wa Umoja wa wazalishaji wa mifuko isiyo na athari kwa mazingira Bw. Sadick Mgonge akitoa maoni ya umoja huo wakati wa Kikao hicho leo.
 Sehemu ya wadau walioshiriki kikao hicho leo Jijini Dar es Salaam wakifuatilia mjadala na maoni ya washiriki .(Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo)


 Frank Mvungi-Maelezo

Wadau wa Mazingira na Wazalishaji wa Mifuko ya Plastiki hapa nchini wameipongeza Serikali kwa kuwakutanisha pamoja ili kujadili kuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki na kutoa maoni yao kwa Serikali juu ya kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira.

Akizungumza wakati akifungua kikao cha wazi cha kupokea maoni ya wadau kuhusu dhamira ya Serikali kupiga marufuku uzalishaji, uuzaji, usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amesema dhamira ya Serikali ni kupata maoni ya wadau na wazalishaji wa mifuko hiyo ili Serikali ifanye tathmini kabla ya kuchukua hatua na kuweka mazingira yatakayowezesha utekelezaji wa Sheria ya Mazingira kwa kila mdau.

“Changamoto imekuwa kubwa katika matumizi ya mifuko ya plastiki katika swala la mazingira kwani tumeshuhudia miundo mbinu yetu ikiathirika, mifugo na hata viumbe vya baharini na kwa mujibu wa tafiti kuna hatari baadae mifuko hii ikawa mingi zaidi baharini kuliko samaki” Alisisitiza Makamba.

Akifafanua Makamba amesema kuwa Serikali imeona ni vyema ikakutana na wadau ili ipate maoni yao kwa kuzingatia kifungu cha 178 cha Sheria ya Mazingira kinachotaka wananchi na wadau kushirikishwa na kupata taarifa kuhusu maswala ya mazingira.

Aliongeza kuwa kuanzia sasa Ofisi yake itakuwa ikishirikiana na wadau katika mambo yote yanayohusu mazingira ili kuongeza tija na kutoa fursa kwa wadau hao kutoa maoni yatakayosaidia katika usimamizi wa Sheria na Kanuni.Naamini kutakuwa na kuvumiliana wakati wa kutoa maoni ili Serikali ipate maoni ya wadau wote kwa ufasaha na hii itasaidia Serikali katika kuchukua hatua ikiwemo kuhakikisha kuwa kuna usimamizi dhabiti wa Sheria ya Mazingira.

Pia Waziri Makamba alilitaka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kusimamia Sheria ya Mazingira kikamilifu ili kulinda rasilimali za Taifa.Kwa upande wake Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Plastiki Tanzania Bw. Ahmed Abdallah amepongeza utaratibu huo wa Serikali kukutana na wadau.

Kumekuwa na maoni mbalimbali kuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki huku baadhi ya wadau wakidai imekuwa na athari kubwa katika mazingira zikiwemo magonjwa, uharibifu wa miundo mbinu na kuleta mabadiliko ya tabia nchi .

No comments

Powered by Blogger.