NAIBU WAZIRI WA NISHATI ASEMA VIJIJI VYOTE TANZANIA BARA KUFIKIWA NA UMEME

 Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameeleza kuwa, Serikali

kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inatekeleza Mradi wa Kusambaza
Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote
ambavyo havina umeme Tanzania bara vitafikiwa na huduma ya umeme.

Ameeleza hayo bungeni, jijini Dodoma tarehe 6 Septemba, 2023 wakati
akijibu swali la Mbunge wa Masasi, Mhe.Geofrey Mwambe ambaye alitaka
kujua ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye Vijiji vya Namikunda,
Chipole, Machombe, Mtakateni, Machenje, Matawale, Mpekeso, Chakama na
Kata ya Temeke.

Akijibu swali hilo, Mhe.Kapinga amesema kuwa katika Jimbo la Masasi,
Mkandarasi NAMIS Corporate Limited alipewa jumla ya vijiji 17 ambavyo
havikuwa na umeme ambapo hadi kufikia tarehe 15 Agosti 2023, vijiji 11
vimeshawashwa umeme na vijiji 6 vitakamilika kabla ya mkataba wa
Mkandarasi kuisha tarehe 31 Desemba, 2023.

Ameongeza kuwa, vijiji vya Namikunda, Mtakateni, Matawale, Mpekeso na
Chakama vimekwishawashwa umeme. Vilevile, hadi kufikia tarehe 31
Desemba 2023, Vijiji vya Chipole na Machombe vitakuwa vimepatiwa
umeme.


Amesema kuwa, kwa sasa, zoezi la kusimamisha nguzo katika Kata ya
Temeke (Mkarango) bado linaendelea na nguzo tayari zimekwisha
simamishwa katika kijiji cha Machenje na zoezi la kuvuta waya
linatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2023.
Mhe. Judith Kapinga

No comments

Powered by Blogger.