SIMBA WAMPOTEZEA MZEE KILOMONI, WAENDELEZA MCHAKATO WA KUMPA TIMU MO DEWJI

Wakati wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa Klabu ya Simba wakiwa wanajipanga kwenda mahakamani kuzuia mikutano ya Klabu ya Simba, upande wa pili uongozi wa klabu hiyo umeonyesha kutojali na unaendelea na mchakato wa kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao na mabadiliko ya kikatiba kama kawaida.
Kupitia taarifa yao kwa vyombo vya habari ambayo Simba imeitoa, imeeleza juu ya mchakato wa kuendeleza mabadiliko kuendelea kama kawaida bila kujali kitisho hicho cha Baraza la Wadhamini wakiongozwa na mzee Kilomoni.
Mabadiliko hayo yanahusisha uendeshaji wa klabu ambapo kumekuwa na taarifa kuwa Mohamed Dewji ‘Mo’ ni mmoja wa wanaowania nafasi ya kuimiliki Simba endapo kutafafanyika mabadiliko ya kikatiba kuhusu uendeshaji na umiliki wa klabu hiyo.
Taarifa kamili ya Simba hii hapa:
TAARIFA KWA UMMA 
Klabu ya Simba inayo furaha kubwa ya kuanza mchakato wa elimu ya mabadiliko ya muundo wa klabu. 
Muundo huo unatokana na mabadiliko ya katiba yaliyofanywa na wanachama na kusajiliwa na msajili wa vilabu nchini. 
Kamati inayoratibu zoezi hilo itaanza kazi hiyo ya utoaji elimu jumamosi hii, kwa kukutana na Wenyeviti wa matawi, kwenye Semina itakayofanyika Makao makuu ya klabu, mtaa Msimbazi kuanzia saa tatu na nusu. 
Semina hiyo ya tarehe tano, itatanguliwa na nyingine zitakazofanyika kwenye wilaya zote za mkoani Dar es salaam, zikuhusisha wanachama wote kutoka kwenye wilaya hizo. 
Pamoja na semina hizo, kamati hiyo pia itatoa elimu kupitia Televisheni,vituo vya Redio na Magazeti,lengo likiwa kila mwanachama wa Simba awe na ufahamu mpana kabla ya mkutano maalum wa katiba wa tarehe ishirini ya mwezi ujao. 
Ratiba kamili ya semina nyingine tutaitoa mwishoni mwa wiki hii. 
IMETOLEWA NA HAJI MANARA
MKUU WA HABARI SIMBA SC *SIMBA NGUVU MOJA*

No comments

Powered by Blogger.