Shabiki wa Yanga: Kwa msaada huu nahamia Simba’

Kufuatia utamaduni uliyojiwekea Simba SC wa kufanya tamasha la klabu hiyo kila ifikapo mwanzo wa msimu safari hii timu hiyo ilifanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kuelekea siku hiyo.
Wiki ya Simba Day ilizinduliwa msimu huu ikiwa na kauli mbiu ya mtaa kwa mtaa kabla ya mchezo wao wa kirafiki Agosti 8 mwaka huu.
Miongoni mwa shughuli zilizofanywa na klabu hiyo msimu huu ni pamoja na kutembelea taasisi hiyo ya (JKCI ) Agosti 7 mwaka huu na kutoa msaada kwa mtoto Mwamvita ambaye alikuwa mgonjwa.
Baba wa Mtoto Mwamvita ahamia klabu ya Simba baada ya mwanae kulipiwa fedha za matibabu katika Simba Week kuelekea Simba Day
Baba mzazi wa mtoto Mwamvita Abdulilah aliyepewa msaada wa matibabu wa Sh 2 milioni na klabu ya Simba katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ameamua kuhama kuishabikia Yanga na kujiunga miamba hiyo ya Msimbazi.
Mwamvita aliyelazwa hospitalini hapo kwa zaidi ya miezi miwili akisubiri upasuaji, alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kushindwa kupumua vizuri kutokana na kuwa na tundu kwenye moyo amepona na anatarajia kuruhusiwa muda wowote kuanzia sasa.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Abdulilah Bakari alisema amehangaika na mtoto huyo kwa takribani miaka mitatu na hivi sasa anashukuru Mungu kwani amepona baada ya kupatiwa matibabu.
“Nashukuru sana kwa dhati Simba, mimi nilikuwa Yanga damu damu, lakini kutokana na kile ambacho Simba wamenifanyia kutoa Sh2 milioni kumtibia mwanangu nimehama rasmi na sasa nimehamia Simba mimi na familia yangu,” alisema Abdulilah.
Naye mtoto Mwamvita alisema anashukuru wanasimba wote kwa kujitoa kuokoa maisha yake.
“Sasa nitaweza kurudi masomoni nashukuru kwa nafasi hii waliyonipa naomba Mungu awaongezee walipopunguza.” Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alielezea Simba News kuwa baada ya kupatiwa fedha za matibabu za Mtoto Mwamvita, walimfanyia upasuaji Agosti 24 mwaka huu.
Alisema upasuaji huo ulifuatia baada ya viongozi na wachezaji wa Simba kutembelea taasisi hiyo Agosti 7 mwaka huu katika maadhimisho ya Simba Day na kukutana na Mwamvita ambaye alikuwa akisubiri kufanyiwa upasuaji.
Kuhusu afya ya Mwamvita, Profesa Janabi alisema kwa sasa anaendelea vizuri na ameshapona tatizo linalomsumbua baada ya kufanyiwa upasuaji.
Mwamvita alifanyiwa upasuaji mkubwa wa kufungua kifua ambapo kwa sasa amepona na anatarajiwa kurudi nyumbani wakati wowote.

No comments

Powered by Blogger.