Madiwani waliojiuzulu wataka kurudi tena CHADEMA
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob (Chadema) amesema kuwa baadhi ya madiwani waliojiuzulu na kukihama chama hicho hivi karibuni wamekiandikia chama hicho barua wakiomba kurejea.
Ameeleza kuwa madiwani hao walirubuniwa kwa ahadi ya fedha ambayo hata hivyo haikutekelezwa kama walivyokubaliana baada ya kujiuzulu.
“Baadhi ya madiwani wametuandikia barua wanaomba kurudi, wanadhani labda wakirudi watarudi kwenye nafasi zao za udiwani kwa sababu ahadi walizokuwa wamepewa za fedha hazikutimizwa,” alisema Jacob.
Kiongozi huyo wa Chadema alidai kuwa kinachofanyika hivi sasa ni siasa za kununua wanachama kama ilivyo kwa vilabu vya soka kununua wachezaji kutoka katika vilabu pinzani.
Alipotakiwa kutoa ushahidi unaoonesha kuwa madiwani hao walipewa fedha na kiasi gani, alisema kuwa wakati wa kufanya mazungumzo walikuwa wanaitwa madiwani kadhaa na watu ambao alidai ni wa chama fulani, lakini baada ya mazungumzo wapo waliokataa mpango huo na kwamba ndiyo walitoa siri za majadiliano hayo.
“Sio kiasi kikubwa cha fedha, wengine waliahidiwa shilingi milioni 10 lakini baada ya kujiuzulu walipewa shilingi milioni tatu. Kuna mwingine aliahidiwa shilingi milioni tatu na zikawekwa benki kabisa, lakini baada ya kujiuzulu fedha hizo ziliondolewa kwenye akaunti yake na benki ikamueleza kuwa aliyeweka ameieleza benki hiyo kuwa aliweka kimakosa hivyo alirejeshewa,” Jacob alidai.
Hata hivyo, alidai kuwa madiwani wa Dar es Salaam ‘hawajanunuliwa’ kwani wengi wanajitambua, wanamsimamo zaidi na wana uwezo wa kifedha angalau usiowafanya kurubuniwa kirahisi.
Jacob alisema kuwa kurejea uchaguzi kwenye kata ambazo madiwani hao wamejiuzulu kutaisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi bilioni kugharamia uchaguzi huku akitamka kuwa Chadema itarejesha nafasi hizo.
Zaidi ya madiwani kumi walijiuzulu nafasi zao miezi michache iliyopita na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi wakieleza kuwa hawakushinikizwa na mtu yeyote bali wameridhishwa na utendaji wa Rais John Magufuli.
Post a Comment