Vinara majimaji selebuka marathon wala shavu la kwenda Sauzi

   Mtoto, Joyce Nzali aliyeibuka kinara wa mbio za watoto 2.5km akivikwa medali na balozi wa Tamasha la Majimaji Selebuka nchini Marekani, Victoria Gorham. Kulia ni mshindi wa pili Rose Kinundo
 Kinara wa mbio za 42km kwa wanawake, Fabiola William akichanja mbuga kwenye Marathon iliyoandaliwa na Tamasha la Majimaji Selebuka linaloendelea mjini Songea, Ruvuma.
                                               Bingwa wa 21km kwa wanawake , Neema Mswadi.
 
Bingwa wa 42km kwa wanawake, Fabiola William kulia akiwa na mshindi wa pili, Neema Kisuda wakihakikisha kama kweli mkwanja waliopewa umetimia. Nyingine akikabidhiwa tuzo na Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Ruvuma, Christian Matembo.
                             Baadhi ya washiriki wa riadha kwenye Tamasha la Majimaji Selebuka mwaka huu

Mwandishi Wetu, Songea

VINARA wa mbio ndefu za 42km, Emmanuel Samson kwa upande wa wanaume na Fabiola William kwa wanawake, mbali na kuondoka na kitita cha milioni moja wamepata shavu la kwenda Afrika Kusini mwakani April kushiriki mashindano ya mbio za Cape Town.
Wawili hao wameokota dodo hilo kwenye mashindano ya Tamasha la Majimaji Selebuka 2017 linaloendelea kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea fursa hiyo ikiwa ni muendelezo wa tamasha hilo kuboresha zawadi kwa washindi. Mwaka jana haikuwepo fursa hiyo.
Aidha kwenye mbio za wanawake, Fabiola alitumia muda wa 2:49:47, nafasi ya pili ni Neema Kisuda muda wa 3:05:29 na fedha taslimu laki tano huku bingwa wa Tokyo Marathon 2002, Banuelia Brighton akishika nafasi ya tatu kwa muda wa 3:13:30 na kuzawadiwa laki tatu.
Kwa wanaume, Samson alitumia muda wa 2:23:28, akifuatiwa na Emmanuel Mpali aliyetumia muda wa 2:24:36 na mkwanja wa laki tano na nafasi ya tatu ikichukuliwa na Mohamed Ramadhani katika muda wa 2:29:27 na kuondoka na kitita cha laki tatu. Mshindi wa nne na tano wakaondoka na mkwanja wa laki mbili na laki moja na nusu. Walioshika nafasi ya sita mpaka 10, waliondoka na 50,000 kila mmoja.
MBIO ZA 21 KM
Kwa upande wa wanaume, nafasi ya kwanza ilishikwa na  Bakari Muna aliyejinyakulia laki nne, akifuatiwa na Mohamed Dude (laki tatu) na Phillip Jacob aliyekuwa wa tatu na kula laki mbili.
Kwa wanawake Neema Mswadi aliwaongoza akifuatiwa na Faraja Emmanuel huku Adelina Fransis akishika ya tatu. Aidha mbio hizo zilishirikisha walemavu (Paralympics) ambako Shukuru Halfan aliwaongoza, akifuatiwa na John Stephen na Matias Jolo kushika ya tatu. zawadi zote zilikuwa sawa na mbio za wanaume; laki nne, tatu na mbili kwa kila kategoria.
10 KM
Samson Limbu aliwagaragaza wenzake kwa upande wa wanaume kwa kushika usukani na kuzawadiwa medali na fedha taslimu laki moja, mkongwe Sanslaus Mina akishika nafasi ya pili akifuatiwa na Leonard Simwa ambako walijinyakulia vitata vya 80,000 na 60,000. Kwa upande wa wanawake, Shakira Abdallah akijimwayamwaya kivyake kwa kukabidhiwa kitita chake cha laki moja kama mshiriki pekee kama ilivyokuwa kwa Agnes John kwenye 5km upande wa wanawake na kupewa 50,000.
2.5 km
Hizi ni mbio za watoto chini wa umri wa miaka 18, ambapo kwa upande wavulana bingwa alikuwa Amos Mapunda, akifuatiwa na Hussein Mwenda na Rahim Haji akishika nafasi ya tatu. kwa wasichana bingwa ni Joyce Nzali, Rose Kinundo akishika nafasi ya pili hukyu nafasi ya tatu ikikaliwa na Janeti Haji.

 Tamasha hilo limepangwa kufanyika tena Julai 14 mwakani

No comments

Powered by Blogger.