INSPEKTA HAROUN: USTAA, UJANA VILINITESA
MOJA kati ya changamoto kubwa inayowakabili mastaa wa fani mbalimbali duniani, ni kuishi maisha ndani ya ndoa. Ni jambo linalowafanya wengi wao kujikuta wakipeana talaka ndani ya muda mchache tu, kuanzia Afrika hadi Ulaya na Marekani.
Mifano ya mastaa walioshindwa kudumu katika ndoa ipo mingi, lakini iliyo karibu zaidi ni ile ya mkongwe wa Muziki wa Afro Pop, Judith Wambura na mtangazaji mahiri, Gardner G Habash ambao baada ya kuoana mwaka 2005, tamati ya maisha yao kindoa yalifikia 2015.
Sababu za mastaa kushindwa kudumu katika ndoa ni nyingi, lakini kubwa inayowatesa ni kushindwa kuzuia presha ya mashabiki wa jinsia tofauti wanaokutana nao kwenye shughuli zao za kila siku.
Inspekta Haroun na mkewe.
Hata hivyo, mmoja wa wakongwe wa Muziki wa Kizazi kipya nchini, Haruna Rashidi Juma Kahena maarufu kama Inspekta Haroun, anaweza kuwa na rekodi ya aina yake, kwani mwaka huu anaingia mwaka wake wa 12 ndani ya ndoa yake na Bahati Shada Msangi.
Inspekta ambaye pia jina lake la kisanii ni Babu, ni kiongozi wa Kundi la Gangwe Mob, moja kati ya makundi ambayo yana mchango mkubwa katika kuufikisha Muziki wa Kizazi Kipya hapa ulipofika.
Akiwa na ‘pacha’ wake, Luteni Kalama, Inspekta anafahamika kwa kazi nyingi alizofanya peke yake, alizoshirikishwa na zile za kundi kama Mtoto wa Geti Kali, Simulizi ya Ufasaha, Nje Ndani, Mzee wa Busara na nyingine nyingi.
Haruna Rashidi Juma Kahena maarufu kama Inspekta Haroun.Pia amewahi kufanya albamu kadhaa binafsi ambazo zilifanya vyema sokoni amb-azo ni pam-oja na Pamba Nye-pesi, Inaba-mba na Ndoa Haina Doa.
Inspekta, mwenyeji wa Mkoa wa Mwanza, ambaye mama yake ni Mzaramo, alizaliwa Mei 5, 1977 Temeke,Dar na kupata elimu yake ya msingi na sekondari hapohapo jijini.
Tarehe yake ya kuzaliwa imekuwa ikimpa matukio mengi muhimu katika maisha yake, kwani aliagana na ukapera Mei 5, 2004 na pia, alizindua albamu yake ya Pamba Nyepesi Mei 5, 2005, kitu kilichomfanya mtangazaji mahiri, Gardner G Habash kumpachika jina la utani la Tripple 5!
“Naona kama nimevunja rekodi, kwani ndoa yangu na mke wangu Bahati hivi sasa tuna miaka 12, kwa msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya bila shaka ni miaka mingi na hamna shaka kuwa nimevunja rekodi.
“Hata hivyo, pamoja na kutimiza miaka yote hii, jua kuwa nimehimili na kuzivumilia changamoto kibao zilizojitokeza miaka yote hiyo, si mchezo,” anasema Inspekta.
Anazitaja changamoto alizokutana nazo ni kwamba hiyo ilikuwa ndoa yake ya kwanza ambayo kwa hulka ya kazi yake ilichangia sana matatizo.
“Unajua nilioa nikiwa staa na ujana ulikuwa mwingi sana, ilikuwa nikichomoka home na washikaji mida ya saa nane mchana, ujue hiyo kurudi home hadi majogoo, kitu hicho kilikuwa kinamkera sana wife lakini sikujali.
“Waandishi nao wakikukuta viwanja upo na washikaji pamoja na mademu zao, wanawapiga picha, wanatupia katika magazeti kwa vichwa vya habari wanavyojua wao, hii ilichangia pia kuipa changamoto ndoa yangu ambayo wengi waliitabiria kuwa haitadumu.
“Pia utakuta unakutana na shabiki wako wa kike, akikuomba kupiga naye picha, ukipiga tu kosa, utajiona siku yoyote ile katika magazeti, ukimkatalia atakuambia unaringa, yaani shida tupu.
“Lakini sasa namshukuru Mungu katika maisha yetu ya ndoa na mke wangu tumejaaliwa kupata watoto watatu ambao ni Hanil, Nassri na Shadya ambao tunaishi nao kwa raha tele,” anasema Inspekta, mmoja wa mastaa waliodumu katika ‘game’ kwa muda mrefu sasa.
“Kuna wasanii mastaa ambao walioa kabla yangu na wengine baada yangu, lakini hivi sasa ndoa zao zimepara-nganyika. Ninamshukuru Mungu kwa hili maana changamoto nilizopitia, bila Mola kunipa hekima mimi na mke wangu tusingedumu,” anasema.
Post a Comment