WABUNGE CUF WALIOVULIWA UANACHAMA KUMSHITAKI PROF. LIPUMBA MAHAKAMANI

Na Regina Mkonde
Wabunge viti maalumu wa CUF wanaodaiwa kuvuliwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho linalomuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, wamedai kuwa hawajapata barua rasmi ya kuvuliwa uanachama. 
Aidha, wakati Prof. Lipumba akitangaza maamuzi hayo mbele ya wanahabari jana, alisema taarifa kuhusu maamuzi ya baraza hilo ya kuwavua uanachama wabunge hao nane kwa tuhuma za kula njama na chadema ili kumuondoa madarakani, zimetumwa kwenda Ofisi ya Spika wa Bunge na Msajii wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya hatua zaidi.
Akizungumza na Mtandao wa Modewjiblog.com mapema hii leo kwa niaba ya wenzake, Riziki Shahali Ngwali amesema, endapo watapata barua rasmi ya kuvuliwa uanachama wao, watakwenda mahakamani kupinga maamuzi hayo kwa madai kuwa Baraza hilo la Lipumba halina mamlaka ya kufanya maamuzi ya chama, kutokana kwamba Lipumba si mwanachama wa CUF.   
“Sisi tutakwenda kutafuta haki katika chombo cha kutoa haki ambacho ni mahakama, tutakwenda mahakamani, kila ngazi ina maamuzi yake lakini kwa Lipumba tunakwenda mahakamani kusema yeye hana mamlaka ya hicho alichokifanya sababu alishavuliwa uanachama. Huwezi ukawa mwenyekiti wakati ulishavuliwa uanachama, na kama si mwanachama huwezi kufanya maamuzi ya chama hayakuhusu,” amesema.
Licha ya hayo, Riziki amedai kuwa, endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) yenye mamlaka ya kuthibitisha wabunge viti maalumu baada ya chama husika kuteua itawapa barua za utenguzi wa uteuzi wao, pia wataenda mahakamani kupinga maamuzi hayo.
“….ndio tunatafuta ushauri wa wanasheria ili watuambie la kufanya, lazima tuhangaike kesho au kesho kutwa sababu na sisi wenyewe hatujapata barua rasmi ya kutuambia hayo maamuzi ya jana, tunayasoma tu kwenye mtandao. Kwa namna yoyote ile tulipewa uteuzi kwenye chama kwa barua, kwa hiyo anayetengua uteuzi wetu atupe barua ya kututengeua, kitu ambacho hakijafanyika,” amesema na kuongeza.
“Lazima tume ndio inahusika zaidi sababu inapitisha wabunge wa viti maalumu baada ya chama kuteua, tume itatujulisha sisi, sababu mkurugenzi wa tume alitupa barua ya uteuzi na hivyo atatupa barua ya kutengua na sababu zake, akitaja sababu na sisi tutafuata ushauri wa sheria tujue tunafanye.”
Kwa upande wake Savelina Mwijage, amedai kuwa Prof. Lipumba amekurupuka katika kufanya maamuzi hayo aliyodai kuwa yamekiuka katiba ya chama hicho kwa lengo la kuendeleza mgogoro ulioko ndani ya chama hicho.
“…Na mimi nimesikia hivyo hivyo, sababu kawaida ukitenguliwa au kusimamishwa unapata barua lakini tunasikia kwenye vyombo vya habari na sijapata barua, na kwa mujibu wa katiba yetu huwezi kuchukuliwa hatua ya kuvuliwa uanachama kabla ya vikao kufanyika, kuna vikao vinakaa vya baraza kuu, kamati tendaji vinakuita mara ya kwanza ya pili mara ya tatu unavuliwa, lengo la kukurupuka hivyo anaendelea na migogoro. Na sisi tutatumia sheria kutulinda sababu kesi iko mahakamani na kwamba  yeye si mwenyekiti,” amesema.

No comments

Powered by Blogger.