TRA, Wajapani waipiga jeki Majimaji Selebuka 2017
Wanafunzi wa Shule ya De Paul wakipokea zawadi kutoka kwa mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica) kwa kuibuka kinara katika mdahalo kwenye Tamasha la Majimaji Selebuka.
Nathan Mpangala akimtunuku mwanafunzi, Lucy Chenji wa Shule ya Sekondari ya Songea Girls wa kuibuka kinara wa shindano la uchoraji vibonzo.
Washindi wa mdahalo kwa shule za sekondari katika Tamasha la Majimaji Selebuka 2017, wakiwa na tuzo zao kwenye picha ya pamoja na majaji wa mdahalo huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Wawili kutoka kushoto ni wanafunzi wa Songea Girls iliyoshika nafasi ya pili, bingwa Shule ya De Paul na Chipole iliyoshika nafasi ya tatu.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya
Mapato Tanzania (TRA) imeongoza washirika wengine kama Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la Japan (Jica) na Chuo Kikuu Huria Tanzania (Open) kulipiga jeki
tamasha la kila mwaka la Majimaji Selebuka kwa kutoa zawadi mbalimbali kwa
shule zilizofanya vema katika shindano la mdahalo kwa shule za sekondari
uliofanyika siku mbili kabla ya kupata washindi.
Jumla ya
shule za sekondari 12 za awali (O-Level) na upili (A-Level), zilichuana vikali
katika mdahalo huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Manispaa ya Songea na
kushuhudia Shule ya Sekondari ya De Paul ikiibuka kidedea kwa kupata alama 42.6
na kutetea taji lao la mwaka jana, ikizibwaga shule za Songea Girls (alama
41.6) na Chipole/St Agness (41.2) zilizoshika nafasi ya pili na tatu, huku
Kigonsela wakishika nafasi ya nne na alama zao 41.1.
Aidha,
katika kutia motisha na hamasa kwa tija ya maendeleo ya elimu mashuleni, TRA
waliwatunuku washindi kitita cha fedha laki mbili kwa bingwa na mshindi wa pili
150,000, mshindi wa tatu 100,000 na wa nne 50,000 huku walimu waliombatana nao
wakila 50,000.
TRA katika
kile kilichotafsiriwa kuvutiwa na mada iliyojadiliwa ya ‘Ulipaji Kodi
hauepukiki kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu’ walikwenda mbali na kuwatuza
wawasilishaji bora na fanisi (best presenter) ambapo Magreth Gama wa Songea
Girls aliibuka kinara na kukunja 150,000. Nafasi ya pili ilichukuliwa na
Sebastino Lubinda (Kigonsela, 100,000) na Monica Shilima wa De Paul aliyeshika
nafasi ya tatu na kuondoka na 50,000.
Nalo shirika la Kimataifa la Maendeleo la
Japan (JICA) walitoa zawadi IPad kwa shule tatu zilizoshinda. IPad hizo zina
notice za masomo yote kuanzia kidato cha kwanza hadi ya sita. Aidha, Chuo Huria
Tanzania (Open) kimetoa zawadi ya fulani kwa shule zilizofanikiwa kuingia
kwenye mchujo wa mwisho.
Wachoraji Bora
Katika
kuhimiza maendeleo shuleni, Balozi wa Tamasha la Majimaji Selebuka, Nathan
Mpangala kupitia Jukwaa la Mtukwao aliandaa shidano la uchoraji vibonzo vyenye
ujumbe wenye kuvuti na nafasi hiyo imechukuliwa na mwanafunzi wa Songea Girls,
Lucy Chenji akifuatiwa na Husna Omar na Wilbard Joseph katika nafasi ya pili na
tatu.
SHULE ZILIZOSHIRIKI:
De Paul,
Songea Girls, Chipole/St Agness, Kigonsela (zilizofika nusu fainali). Nyingine
ni Agustivo, Dr Emmanuel Nchimbi High School, Mfaranyaki, Bombambili, Mashujaa,
Msamala, Londoni na Ruvuma.
Post a Comment