Wananchi wa jimbo la Mhe Lissu wapokea msaada wa Mbunge wa CCM
Mhe Elibariki Kingu
Mbunge wa Singida Magharibi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Elibariki Kingu amewafuta machozi akinamama wa jimbo jirani la Singida Mashariki linaloongozwa na mbunge wa CHADEMA, Mhe Tundu Lissu wilayani Ikungi, Mkoani Singida baada ya kuwanunulia vitanda 52 ili kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto.
Kwa muda mrefu, akinamama hao walikuwa na kilio cha kukosekana kwa huduma hizo, hasa vitanda vya kujifungulia, hivyo kumlilia Kingu aliyeamua kubeba jukumu la mbunge mwenzake.
Kingu amesema ameamua kutoa msaada huo kutokana na maombi aliyoyapata kutoka kwa akinamama wa eneo la Ikungi na pia kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida juu ya kuwasaidia katika sekta ya afya kwa kuwapatia vitanda vya kujifungulia.
“Ni kweli ninatarajia siku yoyote nitakwenda kukabidhi vitanda 86 katika Wilaya ya Ikungi, ambako kuna majimbo ya Singida Magharibi nilipo mimi na jimbo jirani la Singida Mashariki kwa Tundu Lissu, kufuatia maombi ya wananchi hasa akina mama ambao huteseka sana kwa kwenda umbali mrefu kutafuta huduma za afya wakati wa kujifungua,” amesema Mhe Kingu kwenye mahojiano yake na Gazeti la Habari Leo.
Kingu amesema vitanda 86 vyenye thamani ya Sh. Milioni 48.9, vitanda 52 atavigawa katika jimbo la Singida Mashariki na vingine 34 atavigawa katika jimbo lake la Singida Magharibi.
Mbunge huyo wa CCM amesema kati ya vitanda hivyo 52 atakavyovigawa Singida Mashariki, vitanda 26 ni maalumu kwa ajili ya akinamama kujifungulia na vitanda vingine 26 kwa ajili ya wodi za kawaida. Aidha, amesema katika jimbo lake atakabidhi vitanda 34 vya kujifungulia ambavyo kati ya hivyo, vitanda vinne ni vya kisasa vinavyotumia umeme.
Wilaya ya Ikungi ina jumla ya Kata 28 ambapo kati ya hizo, kata 13 zipo katika jimbo la Singida Mashariki ambapo katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 wilaya hiyo ilikuwa na takribani wakazi 272,959.
chanzo; bongo5.com
Post a Comment