POLISI WAWASHAMBULIA NA KUWAUA WAHALIFU WAWILI IKWIRIRI.


 Mkuu wa Oparesheni Maalumu za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas akionyesha kwa Waandishi wa habari silaha mbili aina ya SMG na Shot Gun zilizopatikana baada ya mapambano katika msitu wa Ngomboroni Tarafa ya Ikwiriri ambapo katika tukio hilo waliuwawa wahalifu wawili wanaojihusisha na mauaji katika wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji. Kulia kwake ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Onesmo Lyanga.(Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)
Na. Frank Geofray -Jeshi la Polisi. 
 Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kuwaua wahalifu wawili ambao ni miongoni
mwa wahalifu wanaoendesha mauaji katika Kanda maalumu ya Polisi Rufiji
kufuatia operesheni kali inayoendelea katika Wilaya ya Mkuranga,
Kibiti na Rufiji mkoani Pwani.  Akielezea tukio hilo, Mkuu wa
Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP)
Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilitokea siku ya Jumatano Julai 5
majira ya saa nne usiku katika msitu wa Ngomboroni kata ya Ikwiriri,
Wilaya ya Ikwiriri Kanda maalumu ya Rufiji ambapo askari wa operesheni
maalum wakiwa katika doria za ufuatiliaji wahalifu sugu wanaojihusisha
na mauaji yanayoendelea katika Kanda hiyo ya kipolisi.

Sabas alisema Askari wakiwa na mtuhumiwa mmoja muhimu anayeshiriki katika
mauaji hayo ambaye alikuwa amekamatwa na baada ya mahojiano alikubali
kwenda kuwaonesha Polisi mahali ambapo ni maficho ya wenzake.

Sabas alieleza kuwa, baada ya kufika eneo la msitu wa Ngomboroni kikundi
cha watu wanaokadiriwa kufikia watano walikurupuka kutoka kwenye
kichaka na kuanza kukimbia ndipo askari Polisi kwa tahadhari kubwa
walianzisha mashambulizi na kufanikiwa kumjeruhi mhalifu mmoja kwa
risasi, katika mashambulizi hayo mtuhumiwa aliyekuwa mkononi mwa
polisi naye alijaribu kutoroka na hivyo kupelekea kumjeruhi kwa risasi
hivyo idadi yao kufikia wawili. 

Majeruhi
hao wawili walifariki dunia njiani wakati wakipelekwa hospitali kwa
matibabu kutokana na kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na majeraha ya
risasi waliyoyapata. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha
kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Katika tukio
hilo tumefanikiwa kupata silaha mbili aina ya SMG na shot gun moja
pamoja na risasi tisa za SMG zilizokuwa kwenye Magazine.” Alisema
Sabas. 

Aidha, mkuu huyo wa Operesheni maalum za Jeshi la Polisi Naibu kamishina
Sabas ameendelea kuwasisitiza wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha
kupatikana kwa wahalifu wengine waliosalia na kwamba zawadi nono bado
ipo pale pale na itatolewa kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa sahihi
kuhusiana na wahalifu wanaojihusisha na mauaji katika kanda maalumu ya
Rufiji.

No comments

Powered by Blogger.