MSUVA AITAJIRISHA YANGA SC

                                Kiungo mwenye kasi wa pembeni wa Yanga, Simon Msuva.

KIUNGO mwenye kasi wa pembeni wa Yanga, Simon Msuva amekubali kuachana na Yanga na kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza. Wakati anaondoka, ameifanya Yanga kuwa tajiri baada ya klabu inayomtwaa kukubali kulipa kitita cha dola 80,000 (Sh milioni 177) kwa mkataba wa miaka mitatu.

Fedha hizo, zitaifanya Yanga itulie na kuanza kufanya usajili wa uhakika na ikiwezekana inaweza kupata hata wachezaji watatu au wanne wazuri wa kuisaidia msimu ujao. Klabu hiyo iliyoshika nafasi ya pili msimu uliopita, imekubali kumlipa Msuva mshahara wa dola 4,000 (takribani Sh milioni 9).

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Msuva ameamua kujiunga na Klabu ya Difaa al Jadida ya Morocco ambayo imekuwa ikimuwania kwa takribani miezi mitatu sasa. Msuva anaweza kuondoka nchini ndani ya siku mbili hizi kwenda Morocco kumalizana na klabu hiyo na imeelezwa tayari Yanga imekubaliana nayo. “Kweli kila kitu kimekamilika, Wamorocco wamemalizana na klabu na Msuva ndiyo yuko katika hatua za mwisho.

“Kila kitu kilikwenda kwa mpangilio, ilianza klabu  kwa klabu na baadaye klabu na mchezaji. Sasa mambo yamekamilika,” kilieleza chanzo. Awali Msuva aliliambia gazeti hili kwamba alikuwa na ofa tatu kutoka Morocco, Misri na Afrika Kusini na akasisitiza ataangalia suala la maslahi.

Pamoja na mshahara mnono, Msuva atapata nafasi ya kuonekana katika Ligi ya Mabingwa pia kama ambavyo nafasi angeipata akiwa Yanga lakini timu za Afrika Kaskazini, nyingi hufika mbali zaidi katika michuano hiyo.

Msuva akienda Morocco, ataungana na Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyetarajiwa kuondoka jana usiku kwenda kuungana na kikosi hicho. Maana yake timu hiyo ya Morocco itakuwa imesajili Watanzania wawili kwa wakati mmoja na kama watafanikiwa kupata namba, maana yake wanaweza kucheza wingi zote mbili, ikishindikana basi wanaweza kuchuana wenyewe kwa wenyewe kuwania namba katika kikosi cha kwanza.

No comments

Powered by Blogger.