KUELEKEA MCHEZO WA AFRICAN LYON NA AZAM FC

BAADA ya maandalizi ya takribani wiki tatu, hatimaye Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kesho inatarajia kufungua pazia la mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kukipiga dhidi ya African Lyon, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam saa 10.00 jioni.

Azam FC itaanza ngwe hiyo ikiwa na nguvu mpya kabisa baada ya kufanya usajili mzuri kwenye dirisha dogo la usajili, kwa kuongeza sura mpya tano pamoja na kumrejesha winga wake, Enock Atta Agyei, aliyekuwa kwa mkopo Medeama ya Ghana ilipomsajili, na sasa ataanza kuonekana katika mechi za ligi mara baada ya kutimiza miaka 18 Januari 5 mwakani.

Wachezaji wapya watano waliosajiliwa na Azam FC kwenye dirisha dogo ni beki Yakubu Mohammed (Aduana Stars, Ghana), kiungo mkabaji raia wa Cameroon, Stephan Kingue Mpondo (Coton Sports, Cameroon), winga Joseph Mahundi aliyerejea nyumbani (Mbeya City, huru) na washambuliaji Samuel Afful (Sekondi Hasaacas, Ghana), Yahaya Mohammed (Aduana Stars, Ghana).

Kikosi cha Azam FC kilichomaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 25 tofauti ya pointi 10 dhidi ya vinara Simba (35), kimeonekana kurejea na ari ya juu na morali kubwa kuelekea mzunguko wa pili kutokana na kiwango bora na hali ya kupambana wanayoonyesha kwenye maandalizi mazoezini.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, alisema wamejiandaa vema kuelekea mchezo huo pamoja na mzunguko wa pili wa ligi kiujumla kutokana na nguvu mpya walizoziongeza kikosini.

“Kiufupi raundi ya pili tumejiandaa na timu inanguvu mpya ya wachezaji tuliowasajili ambao hawakuwepo raundi ya kwanza hata mazoezi jinsi yanavyoendelea na jinsi wachezaji wanavyoonekana tunaamini kwa raundi ya pili tutaanza katika mazingira mazuri kuliko ambavyo tulikuwa tukifanya mzunguko wa kwanza,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa wanaingia kwenye raundi ya pili wakijua kuwa kutakuwa na ushindani mkubwa, lakini amekipanga kikosi chake kufanya vizuri huku akiwaambia mashabiki wa Azam FC waendelee kuisapoti timu hiyo.

“Mashabiki waendelee kutusapoti tunajua kwa namna tulivyokuwa tukicehza mzunguko wa kwanza ilikuwa ni ngumu kwao, lakini si kwa wao tu bali ilikuwa kwa watu wote, kwa kile ambacho naweza kuwaambia wajaribu kutuvumilia, mpira tutakaokuwa tunacheza na matokeo tutakayokuwa tunayapata mzunguko wa pili, wenyewe watakuwa wakiyapenda na hawatajutia kabisa kuchagua na kuisapoti Azam FC,” alimalizia.

Rekodi zao (Head To Head)

Agosti 21 mwaka huu, timu hizo zilikutana katika mchezo wa raundi ya kwanza, uliokuwa ni wa tano kihistoria kukutana kwenye ligi, ambapo uliisha kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, Lyon ikitangulia kufunga kupitia kwa Hood Mayanja kwa mpira wa kona wa moja kwa moja kabla ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’, kufunga bao zuri la kusawazisha mwishoni mwa mtanange huo.

Mpaka sasa katika mechi hizo tano walizokutana, Azam FC imeshinda mara tatu, Lyon mara moja huku mchezo mmoja wakienda sare.

Katika mechi zote hizo, Azam FC ndio iliyofunga mabao mengi zaidi ikitupia saba katika lango la wapinzani wao hao, huku Lyon yenyewe ikitingisha nyavu za matajiri hao mara nne tu.

No comments

Powered by Blogger.