Jaji Mutungi Avifutia Usajili Vyama Vitatu vya Siasa Nchini
DAR ES SALAAM: Msajili wa Vyama
vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi leo amevifutia usajili wa kudumu
vyama vitatu vya siasa kwa makosa mbalimbali.
Vyama hivyo vilivyofutwa ni
pamoja na Chama cha Haki na Ustawi wa Jamii (CHAUSTA) kinachoongozwa na
James Mapalala, Chama cha The African Progressive Party of Tanzania
(APPT Maendeleo) kinachoongozwa na Peter Kuga Mziray na Chama cha
Jahazi Asilia kilichokuwa kinaongozwa na Kassim Bakari Ally.
Akiongea na wanahabari leo, Jaji Mutungi
amesema amevifuta vyama hivyo kwa kutumia kifungu cha 19 cha sheria ya
vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992.
Jaji Mtungi ameongeza kuwa, mchakato wa
kufuta usajili wa vyama hivyo unatokana na zoezi la uhakiki wa
utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya sheria ya vyama
vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililofanyika kuanzia Juni 26 hadi
Julai 2016.
Katika zoezi hilo la uhakiki ilibainika
kuwa vyama tajwa hapo juu vimepoteza sifa za usajili wa kudumu kwa
kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa na walipewa taarifa.
Zifuatazo ni sababu za kufutwa vyama hivyo;
Kutokuwa na ofisi ya chama Tanzania Bara
na Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 10 d, kutokuwa na wanachama
Zanzibar kifungu cha 10 b, kushindwa kuweka kumbukumbu za mapato na
matumizi ya chama kifungu cha 14 ( 1) a, kushindwa kuwasilisha hesabu
zake na matumizi ya mwaka kwa mthibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za
serikali kwa mujibu wa vikifungu 14 (1) b (1), kushindwa kuwasilisha
tamko la orodha kwa msajili wa vyama vya siasa mali za chama na mwisho
kushindwa kutekeleza matakwa ya kifungu cha 15 (1) kwamba mapato yote ya
fedha ya chama yawekwe katika akaunti ya chama.
Picha / Habari : Denis Mtima / GPL
Post a Comment