RAIS MAGUFULI AFUTA SAFARI ZA VIONGOZI WA MIKOA NA WILAYA KWENDA BARIADI KUZIMA MWENGE WA UHURU

                                        TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza viongozi wote wa Serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao walishalipwa fedha ya posho na safari kwa ajili hiyo wazirejesh.
 
Taarifa iliyotolewa leo tarehe 12 Oktoba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Rais Magufuli ametoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.

Viongozi waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na Wakuu wote wa Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mameya na Wenyeviti wote wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500.

Kwa kuwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia miaka 17 iliyopita, agizo hilo limewataka Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.

Aidha, Rais Magufuli ameagiza Wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha Mbio za Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.

Hata hivyo Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na Wilaya zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2016.

Mgeni Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Oktoba, 2016

No comments

Powered by Blogger.