Mbowe aikumbuka Oparesheni UKUTA.....Asema Serikali inaendeshwa kwa hila

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema Demokrasia, Katiba na Sheria haziheshimiwi na kwamba  Jeshi la Polisi limekuwa wakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kilichofanywa kwenye uchaguzi wa umeya wa Manispaa ya Kinondoni kinawapa sababu ya kurejea operesheni yao wanayoiita Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA).

Mbowe amesema hayo Oktoba 23, 2016 alipofika eneo ulipofanyika uchaguzo wa Meya Kinondoni ambapo madiwani wa Ukawa walisusia uchaguzi huo na kudai kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Aron Kagurumjuli, ameshirikiana na CCM kuhujumu zoezi hilo, hivyo wametangaza kwenda mahakamani kupinga uchaguzi huo baada ya CCM kuendelea na uchaguzi huo na kutangaza mshindi.

Njama zinazodaiwa kufanywa na mkurugenzi huyo ni kugawanya madiwani kinyume na kanuni kwa kuhamisha madiwani wa upinzani kwenda Halmashauri ya Ubungo na kuwahamishia Kinondoni madiwani wa CCM kutoka halmashauri nyingine.

Mbowe amesema Serikali inaendeshwa kwa hila kwani licha ya uchaguzi kufanyika siku ambayo si ya kazi,  Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, alikataa barua iliyoandikwa na madiwani Jumamosi Oktoba 22 kuzuia uchaguzi huo kwa kudai kuwa si siku ya kazi.

Aliendelea kwa kumlaumu Rais Dk. John Magufuli kwamba ameanzisha utamaduni wa kuuwa demokrasia na kwamba analiletea taifa madhara makubwa.

Kwa upande wake Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema),  amesema wametoka kwenye uchaguzi huo baada ya baadhi ya madiwani wao kuzuiwa kuingia kwenye kikao hicho.

Mdee alisema kuwa  CCM wameingiza madiwani ambao si wajumbe halali wa kikao hicho kwasabau wanatoka katika halmashauri zingine.

“Humo ndani yumo Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na alisajiliwa kama mkazi wa Ilala na alipiga kura za umeya Ilala hivyo mnaweza kuona uhuni unaofanywa.

“Lakini yumo pia Tulia Akson (Dk. Tulia Akson, Mbunge wa Kuteuliwa na Naibu Spika) ambaye si mkazi wa Kinondoni yeye amesajiliwa kama mkazi wa Ubungo,” alisema Mdee.

Amesema kwa mujibu wa kanuni Halmashauri moja haiwezi kuwa na wabunge wa kuteuliwa zaidi ya watatu na kueleza kuwa katika kikao hicho wamo wabunge wanne wa kuteuliwa.

Hivyo, kutokana na hali hiyo Mdee amesema watakwenda mahakamani ili kupata tafsiri za kisheria za suala hilo kupata haki.

chanzo mpekuzihuru.com
 

No comments

Powered by Blogger.