KAMA MASIHARA CHIRWA AMPOTEZA MAVUGO

 MSHAMBULIAJI wa Yanga, Obrey Chirwa ndiye mchezaji pekee ambaye alikuwa gumzo ndani ya kikosi cha Hans Pluijm kuwa ni galasa kwani alikuwa hafungi ila sasa amefanya maajabu yaliyopelekea kumfunika straika wa Simba, Laudit Mavugo ambaye amekuwa Mfungaji Bora mara mbili mfululizo ligi ya Burundi.
Mpaka sasa Chirwa amefikisha mabao manne huku leo akifunga mawili kati ya mabao sita yaliyofungwa na Yanga walipocheza na Kagera Sugar iliyopata mabao mawili pekee, Mavugo yeye amefunga mabao matatu tu. 
Matarajio ya wengi yamekuwa tofauti kwa Mavugo ambaye ndiye aliyekuwa gumzo ndani ya Simba kuwa angeifungia mabao mengi kutokana na uwezo aliouonyesha akiwa na timu yake ya zamani ya Vital'O huku pia akianza ligi kuu ya Vodacom kwa kufunga bao dhidi ya Ndanda tofauti na Chirwa ambaye wengi waliona ni galasa.
Pluijm sasa ameonyesha kuanza kumwamini nyota wake huyo na kumpa nafasi zaidi wakati kocha wa Simba, Joseph Omog yeye ameanza kumpumzisha Mavugo kutokana na kushindwa kupambana zaidi kila anapopata nafasi, Simba wamecheza mechi 10 lakini Mavugo kapewa nafasi mechi tisa ingawa moja dhidi ya Mbeya City alikuwa benchi.
Hivi sasa Chirwa amewafikia nyota kama Amissi Tambwe ambaye ni Mfungaji Bora wa msimu uliopita, Donald Ngoma wote wa Yanga, Rashid Mandawa wa Mtibwa Sugar pamoja na Abdulrahman Musa wa Ruvu Shooting ambao kila mmoja ana mabao manne hadi sasa.
Shiza Kichuya yeye ndiye kinara wa upachikaji mabao akiwa amefikisha mabao saba akifuatiwa na Omary Mponda wa Ndanda FC aliyefunga mabao matano.

No comments

Powered by Blogger.