Mtandao Hatari wa Majambazi Wanaswa Dar
Jeshi la Polisi limedaiwa
kukamata watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha
nzito za kivita ikiwemo bunduki moja kati ya mbili zilizoporwa katika
tukio la kuuawa kwa askari polisi wanne huko Mbande, katika tawi la
benki ya CRDB.
Vitu hivyo vinadaiwa kutumiwa na watu
hao kufanya ujambazi. Inadaiwa kwamba watu hao ni wale waliovamia na
kuiba fedha katika jengo la Sophia House lililopo Keko Dar es Salam
wakiwa wamevaa sare za polisi na kutumia gari ya Noah.
Taarifa kutoka chanzo cha kuaminika
zinaeleza kwamba watu hao ni pamoja na mwanamke mmoja aliyekamatiwa
Bunju katika Manispaa ya Kinondoni ambako vilikutwa vitu vyote
vilivyoporwa na wanaume wawili waliokamatiwa Mbagala Manispaa ya
Temeke, Dar es Salaam.
“Baada ya tukio la Mbande polisi walianzisha operesheni kali ndipo ukasikia yale mapigano kule Vikindu. Kuna watuhumiwa walikamatwa na katika mahojiano ndipo wakaeleza kila kitu,” kimesema chanzo hicho.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kukiri kukusanya silaha kwa kuvamia polisi ili wazitumie baadae katika matukio ya uhalifu, na kukubali kuwapeleka polisi katika ngome yao kuu.
Wakiongozwa na watuhumiwa hao, polisi walikwenda katika nyumba hiyo na wakati wakijiandaa kuivamia wakaanza kushambuliwa ambapo watuhumiwa watatu walijeruhiwa kwa risasi na baadae polisi kufanikiwa kukamata rundo la silaha zikiwemo SMG tatu, bastola 16 na Shotgun Pump Action tatu.
Katika upekuzi zaidi polisi wanadaiwa kukamata risasi 130 za Shotgun, risasi 260 za SMG, risasi 526 za bastola, radio call 12, pingu 48, camera ya usalama (CCTV), panga moja na michimbiko mitatu ya kung’olea mageti.
Hatahivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alipoulizwa kuhusiana na taarifa hizo alisema kuwa atatoa ufafanuzi siku ya leo.
Tangu kuuawa kwa askari wanne huko Mbande, Jeshi la Polisi limekuwa likitekeleza operesheni zake za kuwatafuta wahusika na kupambana na matendo hayo kwa usiri mkubwa huku Kamishna Sirro akiahidi kutoa taarifa pale Jeshi hilo litakapohitaji kuwasiliana na Umma.
Post a Comment