Matapeli watinga Yanga, waharibu mifumo
Kikosi cha timu ya Yanga.
Sweetbert Lukonge, Dar es SalaamKLABU ya Yanga imepata pigo baada ya hivi karibuni watu waliotajwa kuwa ni matapeli, kuvamia na kuharibu kabisa mfumo wa mawasiliano wa klabu hiyo ambao ulikuwa ukitumika kwa ajili ya kuwapasha habari wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.
Kwa mujibu wa habari ambazo zimelifikia gazeti hili kutoka katika Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha klabu hiyo, watu hao wasiojulikana walivamia akaunti rasmi za kijamii za klabu hiyo na kuharibu mfumo mzima wa mawasiliano kwa kufuta kumbukumbu zote kwenye akaunti hizo.
Akaunti za klabu hiyo zilizovamiwa na watu hao ni zile za mitandao ya kijamii ya Fecebook na Instagram iliyokuwa ikijulikana kwa jina la @yangasc ambazo zilikuwa zikitumika kwa ajili ya kuwafikishia taarifa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.
“Imetusikitisha sana kwani ni jambo la ajabu sana lakini tayari uchunguzi wa jambo hilo umeshaanza na baadhi ya watu waliohusika na suala hilo tumeshawabaini na inaonekana walifanya hivyo kwa chuki zao binafsi ambazo kimsingi hazina nia nzuri na klabu yetu.
“Hata hivyo, kila kitu kitakapokuwa sawa basi tutawataja watu hao ambao baadhi yao waliwahi kuwa viongozi wa klabu yetu,” alisema kiongozi huyo ambaye aliomba kutotajwa jina lake kutokana na sababu mbalimbali alizozitoa ambazo gazeti hili liliziona kuwa ni za msingi.
Hata hivyo, alipoulizwa juu ya suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, alikiri kutokea kwa jambo hilo na kudai kuwa jitihada za kufungua akaunti mpya zimeshafanyika lakini pia wanaendelea na uchunguzi wa kuwabaini wale wote waliofanya jambo hilo ili waweze kuwafikisha katika mkono wa sheria.
Post a Comment