Makonda akanusha kuagiza msako nyumba za wageni mchana kweupe ‘serikali haiendeshwi na umbea’
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekanusha tetesi kuwa
ametoa agizo la watu wanaolala kwenye nyumba za wageni wakamatwe nyakati
za mchana na kudai kuwa serikali haiendeshwi kwa umbea.
Amekanusha uvumi huo uliosambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao
mbalimbali ya kijamii na kuviasa vyombo vya habari kutoa habari zenye
uhakika.
“Hili suala mimi nimelisikia katika namna ambayo hata mimi mwenyewe
nimebaki nashangaa,” alisema Makonda. “Moja aliyetoa maelezo anasema
nina umbea maana yake kwanza ni mmbea,kwasababu mbea lazima awe mbea.
Lakini serikali haijawahi kufanya kazi kwa namna hii, serikali haiwezi
kuendeshwa kwa njia ya umbea. Haiwezekani mtu anakaa kwenye gari yake
anaanza kurekodi anatuma anaanza kuhangaisha vichwa vya watu wazima.
Kwahiyo hata baadhi ya vyombo vilivyokwisha kuandika na baadhi ya watu
kujadili ni kwamba wanajadili umbea ule ule tu. Ni namna pekee nzuri ya
kupata wambea kwasababu ukiwa mbea utahangaika usiku na mchana kutafuta
umbea, lakini serikali haifanyi kazi kwa umbea,” alisisitiza Makonda.
“Lakini la pili kufahamu ambalo ni jambo jema ni kwamba kabla ya
kufanya maamuzi ya kuandika habari au kutangaza habari ni vema pia
ukaonana na mamlaka husika, anasema polisi maana yake lazima kamanda
Siro aulizwe na atoe taarifa, Je ni kweli kuna maagizo kama hayo? Lakini
jambo jingine kama ni wakuu wa wilaya je kweli wakuu wa wilaya
wamepokea maagizo kama hayo? Na hata kama ni mkuu wa mkoa je kuna
maagizo kama hayo? Ukweli ni kwamba hakuna maagizo ya namna hiyo uamuzi
wa mtu kupumzika ama kulala ni muda wowote ule. Wako watu wanafanya kazi
ya ulinzi, wapo watu wanafanya kazi viwandani, wako watu wanasifiri na
kuingia Dar usiku wa manane, kila mtu ana haki ya kupumzika na kila mtu
ana haki ya kuwa na faragha yake, na ndiyo maana kukawepo na nyumba za
kulala wageni.”
Aidha Makonda alitoa ufafanuzi wa suala la ukaguzi, “Sasa suala la
ukaguzi au kama kuna maeneo wameonekana polisi wakifanya ukaguzi ni
jambo jepesi tu. Nenda kwenye kituo husika utapewa maaelezo, na
inawezekana labda wametilia shaka lakini ikumbukwe hivi karibuni askari
watano wamepoteza maisha yao, sambamba na hilo juzi tumekamata silaha za
kutosha na nyie mnafahamu, bastola zaidi ya 15,SMG zaidi ya nne na
risasi nyingi sana na zimekamtwa kwenye majumba ya watu, inawezekana
kuna baadhi ya maeneo wameyashtukia wakaona kuna haja ya kufanya
upekuzi. Lakini si maelekezo zaidi ya usalama wa raia wote wanaoishi
mkoa wa Dar es Salaam, hasa ikumbukwe kipindi cha nyuma nilisema
wenyeviti wa mitaa wahafahamu wananchi wanaoishi nao, watu
walilibadilisha jambo jingine,” alifafanua.
Pia amewataka wakazi wa Dar es Salaam watambue jambo hili, “mimi
niwaombe wananchi wanaoishi mkoa wa Dar mamlaka zipo, viongozi wapo,
hakuna mtu aneweza kubugudhiwa, cha msingi kila mtu aishi kwa utaratibu,
sheria na kanuni, hatuwezi kuishi kwa maelekezo ya kila siku, tunaishi
kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni, taarifa zipuuzeni, na kwa
bahati nzuri mmepata mkuu wa mkoa ambaye akiwa na jambo lake atalisema
hadharani, hana sababu ya kumungu’nya maneno.”
“Wanaofanya kazi ya umbea waendelee, na tunaofanya kazi ya kujenga
mkoa wetu tuendelee kujenga mkoa wetu kwa amani, upendo na
mshikamano,na wanaofanya majungu na siasa waendelee, tunaofanya kazi za
maendeleo tuendelee na mwisho wa siku Oktoba tarehe moja ni siku ya
kupanda miti.”
BY: EMMY MWAIPOPO
credit bongo5
Post a Comment