Mabaki yaliyopatikana Pemba, ni ya MH370
Mabaki ya ndege yaliyopatikana katika pwani ya visiwa vya Pemba nchini Tanzania yalitoka kwa ndege ya shirika la Malysia Airlines iliyotoweka mwaka 2014, maafisa wa Malaysia wamethibitisha.
Waziri
wa uchukuzi wa Malaysia Liow Tiong Lai amesema kupitia taarifa, kwa
mujibu wa shirika la habari la Reuters, kwamba baada ya uchunguzi
imebainika kwamba kipande hicho kikubwa cha bati kilichopatikana mwezi
Juni ni cha ndege hiyo safari nambari MH370.
Amesema
uamuzi huo ulifikiwa na wataalamu kutoka Idara ya Usalama wa Safari za
Ndege ya Australia (ATSB) na wale wa kuchunguza usalama wa MH370.
Mapema
Julai, waziri wa uchukuzi wa Australia Darren Chester alikuwa amedokeza
kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa mabaki hayo yalikuwa ya ndege hiyo.
Alisema muundo wa mabaki hayo, ukubwa wake na muonekano wake viliashiria kwamba yalikuwa ya ndege hiyo ya Malaysia.
Mabaki
hayo pia yalikuwa na muhuri wa kuonesha tarehe ya kuundwa kwake ambayo
ilikuwa Januari 23, 2002. Ndege hiyo ya Malaysia iliwasilishwa kwa
shirika hilo 31 Mei, 2002, kwa mujibu wa tovuti ya shirika la Channel
News Asia.
Ndege
hiyo aina ya Boeing 777 ilitoweka Machi 2014, ikiwa na abiria 239 baada
ya kupaa kutoka Kuala Lumpur, mji mkuu wa Malaysia kuelekea Beijing.
Bw
Liow amesema mabaki hayo yatachunguzwa zaidi kubaini iwapo kutapatikana
ufumbuzi kuhusu kilichotokea hadi ndege hiyo ikatoweka.
Awali,
wachunguzi walikuwa wamethibitisha kwamba mabaki yaliyopatikana visiwa
vya Reunion mwezi Julai 2015 yalitoka kwa ndege hiyo.
Mabaki mengine yanayodhaniwa kutoka kwa ndege hiyo yamepatikana Msumbiji, Afrika Kusini na visiwa vya Rodrigues, Mauritius
Chanzo BBC
Post a Comment