CUF Waondolewa Kupisha Mkutano wa Rais Magufuli Pemba
Jeshi
la Polisi Wilaya ya Chakechake, Pemba limezuia kufanyika mkutano na
vyombo vya habari wa Chama Cha Wananchi (CUF) uliokuwa umepangwa
kufanyika leo wilayani humo, kupisha ziara ya Rais John Magufuli
itakayoanza leo.
Rais Magufuli anatarajia kuanza leo ziara yake ya kwanza visiwani humo tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Ikulu, Rais Magufuli atazulu Pemba leo na kesho atakuwa Unguja.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Shekhani Mohamed Shekhani amesema kuwa
zuio hilo la mkutano wa CUF ni kwa sababu eneo wanalotarajia kutumia
liko jirani na eneo la uwanja atakaokuwa akihutubia Rais Magufuli.
Hata
hivyo, Katibu wa CUF wilaya ya Chake Chake, Saleh Nassor Juma
alilalamikia maamuzi hayo ya Jeshi la Polisi kwa madai kuwa wao walitaka
kufanya mkutano na vyombo vya habari na sio mkutano wa hadhara. Alisema
kuwa tayari walishawaeleza Idara ya Habari Maelezo na waliridhia.
Alisema
mkutano huo na waandishi wa habari ulilenga katika kutoa tamko lao
kuunga mkono uamuzi uliochukuliwa na Baraza Kuu la chama hicho
kumsimamisha uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim
Lipumba pamoja na viongozi wengine 10.
“Niliwakatalia
kwa hoja kwamba mkutano na waandishi wa habari ni haki yetu ya kikatiba
na tulikwishawataarifu watu wa Idara ya Habari Maelezo juu ya kikao
hicho halali ambacho wao pamoja na waandishi wa habari walithibitisha
kuwa watahudhuria,” alisema Nassor.
Idara
ya Habari Maelezo ilithibitisha kuwa walikubali kufanyika kwa mkutano
huo wa CUF na vyombo vya habari lakini baadae walipokea taarifa ya
kuahirisha kupisha ugeni wa Rais Magufuli.
Post a Comment