RAIS MAGUFULI AKERWA NA UOZO ULIOPO NDANI YA CCM.......AAGIZA JIJI LA MWANZA LISIWATOZE KODI WAFANYABIASHARA WADOGOWADOGO
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama
cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuna mambo ya hovyo
ambayo yapo ndani ya Chama cha Mapinduzi ambayo yanahitaji kuhojiwa na
kupatiwa majibu yenye tija.
Aikihutubia maelfu ya wananchi jana waliojitokeza kumsikiliza katika viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza Dkt. Magufuli alisema
anafahamu kwamba ndani ya CCM kuna mambo ya hovyo na mfano ni uwanja wa
CCM Kirumba na majengo mengine ya CCM ambayo ukiuliza maduka na ofisi
zinazozunguka majengo hayo mapato yake yako wapi huwezi kupata majibu ya
kuridhisha.
"Ninyi
wananchi wa Mwanza na wanachama wa CCM hojini haya na atakayewauliza
mwambieni ni mimi Mwenyekiti wa CCM nimesema muwaulize, nataka chama
ambacho mali zake zinajulikana kwa sababu ukienda kuwauliza mnakusanya
shilingi ngapi kwa chumba kimoja wanaweza kukuambia ni elfu 50 kumbe
wanaingiza laki 5" Alisema Rais Dkt. Magufuli
Rais Magufuli alisisitiza
kwamba anaitaka CCM ya Rais wa kwanza wa Tanzania Mwl. Julius Nyerere
siyo CCM ya watu ambao mchana wapo CCM na usiku wapo vyama vingine,
wanaofanya hivyo ni bora wahamie huko moja kwa moja.
Aidha
katika hatua nyingine Rais Dkt. Magufuli ameagiza uongozi wa Jiji la
Mwanza kutowatoza ushuru wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwa wanatakiwa
wanufaike na taifa lao na pia wamachinga waachwe mjini kwanza hadi hapo
watakapo andaliwa mazingira mazuri ya kufanyia biashara yatakayokuwa na
wateja.
Post a Comment