Ndege za Kivita Kutawala Anga la Dar Septemba 1
Septemba
mosi mwaka huu inataraji kuingia katika histori ya Tanzania kutokana na
matukio ambayo yanataraji kufanyika siku hiyo, matukio hayo ni pamoja
na sherehe za miaka 52 ya Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ),
maandamano ambayo yamepangwa kufanywa ya UKUTA na tukio la kupatwa kwa
jua.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati alipokutana na Maafisa wa Jeshi la JWTZ
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema JWTZ inapotimiza
miaka 52 ni fahari kubwa hivyo tunapaswa kuwapongeza kwa kudumisha amani
na mshikamano.
Alisema
Jeshi hilo limejipanga kurusha angani ndege zake za kivita katika anga
la Dar es Salaam, Septemba 1 mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho
ya miaka 52 ya kuanzishwa kwake.
Makonda aliwataka wananchi kutokuwa na hofu wanaposikia ngurumo za ndege hizo bali wafurahie kwani ni ndege zao.
“Mnaposikia
milio ya ndege zetu mbalimbali, mfurahie kwa sababu hizo ni ndege za
wananchi. Usisikie muungurumo ukashtuka. Hakuna jambo lolote lile zaidi
ya kuonesha vifaa vyetu na jinsi ambavyo wanajeshi wetu kwa miaka 52
wamaeendelea kuwa imara na vifaa vizuri,” alisema Makonda.
Aidha,
Mkuu huyo wa Mkoa waliwataka wananchi waliojipanga katika vikundi
mbalimbali kuripoti kwa wakuu wao wa wilaya kujiandikisha ili waweze
kushiriki pamoja na Jeshi hilo katika zoezi la usafi jijini humo.
Aliwataka
wakazi wa mkoa huo pia kujitokeza kuchangia damu katika vituo
mbalimbali ambavyo vimeanishwa ili kuunga mkono juhudi za uchangiaji
damu zitakazofanywa na wanajeshi wa JWTZ.
“Hii
ni sehemu ya amani, tufanye usafi kwa amani. Tujitolee damu zetu kwa
amani na mwisho wa siku tuwaenzi na kuwapongeza wanajeshi wetu kwa kazi
kubwa wanayoifanya,” Makonda alieleza.
Katika
hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa aliendelea kutoa onyo kwa watu
watakaotaka kufanya maandamano yaliyopigwa marufuku ya oparesheni UKUTA
akiwataka kutii sheria.
“Mimi
ninavyojua UKUTA ni kuwa mtu amefika mwisho wa kufikiri sasa kama
watakuwa wamefika mwisho wa kufikiria basi sisi tutawasaidia … watu wapo
wanapanga kufanya mambo ya kusaidia jamii wao wanapanga maandamano
nawashauri wananchi waungane na Polisi,” alisema Makonda.
Post a Comment