Lowassa, Mbowe na Katibu Mkuu Chadema Waanza Mikakati ya UKUTA
Siku moja baada ya Chadema kutangaza safu ya Ukuta, viongozi wa chama hicho wameanza kutawanyika mikoani kuanza kutoa elimu ya mpango huo.
Wakati
mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akiwa Kanda ya Kaskazini
aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa alikuwa mkoani Mbeya
na jana alishiriki ibada na kuanza vikao vya mkakati huo.
Mbowe jana
alikutana na viongozi wa kanda hiyo na kuunda kamati zitakazokwenda
katika majimbo yote 35 ya uchaguzi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,
Tanga na Manyara kutoa elimu.
Mbowe alisema katika kikao hicho, ambacho
ni mfululizo wa vikao vinavyoendelea kanda zote nchini, wamekubaliana
kutoa elimu ya dhana ya Ukuta.
Hata hivyo, alisema bado chama hicho
kimetoa fursa ya mazungumzo kwa taasisi yoyote ili kuhakikisha mgogoro
uliosababisha Kamati Kuu kuunda Ukuta.
Wakati Mbowe akisema hayo, Lowassa
ametua katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayojulikana kama Kanda ya
Nyasa akiwa na mambo matatu makubwa.
Aliwasili jana asubuhi kwa ndege ma
kwenda moja kwa moja kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Usharika wa Forest akiwa na viongozi wa chama hicho wa kanda
pamoja na wabunge mbalimbali wa majimbo ya mikoa ya Mbeya, Njombe,
Iringa, Songwe, Rukwa na wale wa viti maalumu.
Waziri Mkuu huyo wa
zamani, alishiriki ibada ya kawaida na alipokea zawadi ya nyimbo
zilizowekwa kwenye ‘flash’ kutoka kwa wanakwaya wa kanisa hilo huku naye
akiwachangia kwa kuendesha harambee ya papo kwa papo kutoka kwa
viongozi alioongozana nao.
Katika harambee hiyo, zilipatikana Sh4
milioni zikiwamo Sh 1 milioni ambazo aliahidi kuzitoa.
Kabla ya ibada
kumalizika, Lowassa na ujumbe wake waliondoka kwenda kwenye kikao cha
Baraza la Chadema la Kanda.
Katibu wa Kanda hiyo, Frank Mwaisumbe
alitaja mambo matatu makubwa kutoka kwa Lowassa kuwa la kwanza alihimiza
wanachama wote kuimarisha umoja na kufuta mipasuko iliyotokea wakati wa
uchaguzi.
Pili, aliwasihi wana Chadema wote kuwa jasiri kwa kupigania
haki na kujitambua na la tatu ni kujiandaa kwa Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa utakaofanyika 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Mwaisumbe alisema
baada ya kikao cha jana, leo Lowassa anaanza kutembelea majimbo ambako
atakuwa na vikao vya ndani katika majimbo ya Mbeya Vijijini, Mbozi na
Tunduma na kesho atakuwa kwenye majimbo ya Nkasi Kaskazini na Kusini na
Sumbawanga wakati kesho kutwa atakuwa Mbarali, Makambako, Njombe Mjini
na Mafinga. Agosti 25 atakuwa Iringa Mjini na Kolo.
Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Vincent Mashinji yupo Kanda ya Serengeti inayojumuisha
mikoa mitatu; Simiyu, Shinyanga na Mara na jana aliwataka Watanzania
kuwapuuza watu wanaodai chama hicho kimejipanga kufanya vurugu Septemba
Mosi akisisitiza kuwa maandamano yatakayofanyika ni ya amani.
Alisema
kamwe hawawezi kuvunja sheria na Katiba ya nchi na kwamba kinachofanyika
kipo kwa mujibu wa sheria.
“…Nawaomba Watanzania wote watuunge mkono
maana tunachokwenda kukifanya ni kwa ajili ya kuwanusuru watoto wetu
wasiingie kwenye matatizo maana kinachoendelea kinakwenda kuondoa
demokrasia na utawala bora,” alisema.
Post a Comment