DAKIKA 120 ZA MAVUGO SIMBA NOMA SANA ...ATUA NA KUKABIDHIWA JEZI


SIMBA sasa imekamilika. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya mshambuliaji wake mpya raia wa Burundi, Laudit Mavugo kuonyesha vitu adimu katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam kwa muda wa dakika 120. Mavugo alitua nchini juzi Alhamisi akitokea Burundi ambako alikuwa akiitumikia timu ya Vitalâ O inayoshiriki ligi kuu ya nchi hiyo na amekuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo ambapo msimu wa 2014/15 alifunga mabao 32 wakati msimu uliopita wa 2015/16 alifunga mabao 30. Katika mazoezi hayo ambayo yalikuwa ni ya kwanza kwake akiwa na kikosi cha Simba lakini pia kwa timu kufanya jijini Dar es Salaam tangu ilipotoka kambini Morogoro, Mavugo alionyesha kuwa si mchezaji wa kubahatisha kutokana na uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga pasi, kukimbia na mpira lakini pia kupiga chenga. Beki wa kulia wa timu hiyo, Hamad Juma na straika Frederic Blagnon kwa wakati tofauti walikumbana na balaa kutoka kwa mshambuliaji huyo baada ya kupigwa chenga za hatari jambo lililosababisha watu wote waliokuwa uwanjani hapo wampigie makofi Mrundi huyo. Hali hiyo, pia ilimpagawisha kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog ambaye alimuita msaidizi wake, Mganda, Jackson Mayanja kisha wakaanza kujadiliana wakati mazoezi yakiendelea. Hata hivyo, baada ya mazoezi hayo, Omog aliliambia Championi Jumamosi: Namshukuru Mungu kikosi changu hivi sasa kipo vizuri na tunaendelea na mazoezi yetu kama kawaida, hata hivyo leo hii nimepata mshambuliaji mpya kutoka Burundi na kazi yake nimeipenda. Kwa siku ya kwanza tu ameonyesha uwezo hivyo ni matumaini yangu kuwa kadiri siku zinavyoenda basi anaweza kuwa msaada mkubwa kwetu ila nitamfuatilia zaidi katika mazoezi ya kesho (leo). Mavugo ametua Simba akiwa tayari ameshasaini mkataba wa awali, hivyo jana au leo Jumamosi anatarajiwa kuingia mkataba rasmi wa kuitumikia klabu hiyo. Ukiachana na Omog, mashabiki wa timu hiyo pia nao walimsifia Mavugo ambaye walikuwa wakimsubiri kwa hamu kubwa ajiunge na timu hiyo tangu msimu uliopita lakini ikashindikana. Mashabiki hao walimfuata na kumwambia kuwa kazi yake wameikubali hivyo watahakikisha wanashirikiana naye kwa kumuunga mkono ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri msimu ujao. Wachezaji kama huyu ndio tunaotaka, anakuja siku moja na anaonyesha uwezo, hakika safari hii watatukoma kwani kikosi kimekamilika, Mavugo piga kazi tupo nyuma yako,alisikia akisema maneno hayo mmoja kati wa mashabiki wa Simba waliokuwa uwanjani hapo. Akizungumza na gazeti hili baada ya mazoezi, Mavugo alisema: Nimekuja Simba kufanya kazi na siyo kutembea, hivyo nitahakikisha natumia nguvu zangu zote ili tuweze kuibuka mabingwa.Najua kuwa timu hii haijachukua ubingwa kwa muda mrefu lakini kwa jinsi kikosi nilivyokiona kwa haraka hakika sioni kama kutakuwa na timu ya kutuzuia, hata hao Yanga ambao ni mabingwa hawana wachezaji wenye vipaji kama hawa niliowaona hapa.Aliongeza: Kama Amissi Tambwe amekuwa akifunga mabao mengi kwa nini mimi nisifunge? Nawaambia Wanasimba kuwa Mungu akinijalia uzima, natarajia kufunga zaidi ya mabao 30 kama nilivyokuwa Burundi, hivyo naomba ushirikiano wao tu wa kutuunga mkono tunapokuwa uwanjani, kwani wao ni wachezaji wa 12. Kwa nini msimu uliopita hakutua Simba? Katika hilo viongozi wa Simba hawapaswi kulaumiwa ila mimi ndiye niliyekuwa na makosa lakini siwezi kusema ni makosa gani hayo. Nachoweza kusema ni kwamba nashukuru Mungu safari hii nimefanikiwa kuja na nitaitumikia Simba kwa moyo wangu wote kwa sababu ninaipenda tangu nikiwa mdogo, mambo yaliyopita naomba tuyaache, tugange yajayo

No comments

Powered by Blogger.