MBOWE AHOJIWA NA KUACHIWA KWA DHAMANA.......TUNDU LISSU ASISITIZA OPARESHENI UKUTA IKO PALEPALE


MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema licha ya viongozi wa chama hicho kutishwa, kukamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi, bado msimamo wao kuhusu operesheni Ukuta itakayofanyika Septemba Mosi mwaka huu uko pale pale.

Chama hicho kinatarajiwa kufanya operesheni mpya iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta).

Operesheni hiyo inatarajiwa kuwa itakwenda sambamba na uzinduzi wa mikutano ya hadhara nchi nzima, ambayo itafanyika Septemba Mosi, mwaka huu.

Hatua hiyo imefikiwa na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi kwa siku nne mfululizo wiki iliyopita jijini Dar es Salaam na kutoa maazimio matatu ambayo yatatekelezwa na chama hicho.

Pamoja na mambo mengine, chama hicho kimesema lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini, kiliyodai kuwa yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam baada ya kuhojiwa na kuachiwa kwa dhamana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwanasheria  Lissu alisema msimamo wao uko palepale na hakuna kilichobadilika.

“Wamemuhoji kwa taarifa aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama wa kufanya mkutano nchi nzima. Tatizo jeshi letu wakisikia maandamano, mkutano au mtu anamsema Magufuli basi anatuhumiwa kwa uchochezi, wametumia muda mrefu kumuhoji lakini mwisho wamemwachia kwa dhamana na amewahi ‘Airport’ ili aende kuhudhuria mazishi ya kamanda wetu Senga (Joseph) na watamwita watakapomwihitaji tena,” alisema Lissu.

Alisema pamoja na hayo bado msimamo wa chama hicho kufanya mikutano waliyoiita Operesheni Ukuta ipo pale pale ifikapo Septemba Mosi, mwaka huu.

“Nafikiri ni muhimu sana huko tunapoenda kuzungumza na wenzetu hii kitu inaitwa uchochezi ni nini? Tunashitakiwa kwa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo waliingiza vifungu vya uchochezi mwaka 1978 lengo lao kuu ni kuwafunga watu midomo na ilitungwa wakati wa mfumo wa chama kimoja.

“Hata hivyo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ndiye wa kwanza kushtakiwa kwa uchochezi  pamoja na mwandishi Robert Makenge na mwenzao Rashid Bagedae, kwa msingi huo sisi tunafuata nyayo zake,” alisema.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema kuitwa mchochezi, ni jambo la ufahari kupinga udikteta kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.

“Nasema hivyo kwa sababu Mwalimu Nyerere ndiye wa kwanza kuitwa mchochezi, ni kitendo cha kufunga watu midomo ili washindwe kuwaita watu wajinga pale wanapofanya ujinga.

“Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1992 wakati mfumo wa vyama vingi unatambulishwa na kuanza nchini ilipendekezwa sheria hii ifutwe kwa sababu haiendani na mfumo uliopo lakini hakuna kilichofanyika,” alisema.

Mwanasheria huyo ambaye naye amefunguliwa kesi ya uchochezi katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar, aliwataka wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi Agosti 2, mwaka huu mahakamani hapo.

“Dawa yao si majaji bali umma… umma ufurike, tutawashinda hawa watu makesi yenyewe ni haya ambayo hayana kichwa  wala miguu,” alisema na kushangiliwa na wafuasi wa chama hicho.

Mbowe alifika kituoni hapo akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwamo Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa ambaye hata hivyo alizuiwa kuingia katika chumba cha mahojiano.

Askari waliokuwa kwa wingi katika eneo hilo, walisikika wakisema kuwa anayepaswa kuingia ndani ni Mbowe, Mwanasheria Tundu Lissu na Wakili wa Chadema, John Mallya.

Lowassa, wafuasi wa Chadema na waandishi wa habari walilazimika kubaki nje huku askari wakiimarisha ulinzi wakiwa wamebeba bunduki zao huku magari yenye maji ya kuwasha yakiwa yameegeshwa pembeni.

Wakati chama hicho kikijiandaa kutekeleza Operesheni Ukuta Septemba Mosi, tayari Rais Magufuli amezuia operesheni hiyo na kuwaonya wale wote watakaokaidi agizo lake na kuamua kuandamana.

No comments

Powered by Blogger.