MSUVA: LUGHA NI TATIZO KWANGU MOROCCO
Simon Msuva akikabidhiwa jezi.
KADIRI siku zinavyokwenda, matajiri wa timu ya Difaa El Jadidi ya Morocco waliopata nafasi ya kumnasa nyota wa Yanga, Simon Msuva, wameendelea kuvutiwa na kiwango chake.
Kutokana na kuwa hatari kwenye kufunga mabao, kocha wa timu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo, Abderrahim Taleb, amelazimika kumbadilishia namba, amemtoa winga na kumchezesha kama namba kumi.
Msuva ambaye amejiunga na klabu hiyo mwezi uliopita kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Yanga, ameendelea kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Difaa kutokana na uwezo wake na kasi aliyonayo.
Msuva alianza kuwakosha mashabiki wa timu hiyo mapema, kwani katika mechi yake ya kwanza, siku moja tu baada ya kutua, alifunga, na sasa ana mabao saba katika mechi 10.
Kabla ya kuondoka Yanga, Msuva alikuwa ni mchezaji muhimu kikosini hapo ambapo msimu u l i opita aliibuka kinara wa ufungaji kwenye Ligi Kuu Bara akifunga mabao 14 sambamba na straika wa Ruvu Shooting, Abdulrahman Mussa.
Championi Jumatatu limemtafuta Msuva na kufunguka mambo kadhaa ya maisha yake ndani na nje ya klabu hiyo.
C HAMPIONI : Unaweza kutueleza mapokezi yako baada ya kutua Morocco yalikuwaje?
MSUVA: Kiukweli mapokezi yangu hadi sasa ni mazuri kiasi kwamba inafikia wakati najihisi kama niko nyumbani kabisa maana wachezaji na viongozi wangu wananipenda sana.
CHAMPIONI: Kwa sasa unaishi kambini au umepangishiwa nyumba?
MSUVA: Hapa kwa sasa naishi katika nyumba yangu mwenyewe ambayo nilikabidhiwa na klabu yangu baada tu ya kufi ka hapa Morocco.
CHAMPIONI: Unahisi mashabiki wa Difaa El Jadidi na makocha wako kwa jumla wanakuchukuliaje tangu uanze majukumu yako?
MSUVA: Kiukweli naona wananizungumzia kwa mambo mazuri tu na hicho ndicho kitu pekee ambacho namshukuru sana Mungu kwani hamasa na mwamko wanaonionyeshea ni mkubwa sana kwangu, hivyo inafikia hatua naona kama nilichelewa kuja huku.
CHAMPIONI: Tangu umeanza kutekeleza majukumu yako unaona kuna tofauti ipi na Tanzania?
MSUVA: Tofauti zipo maana huku ni nje ya nchi yangu niliyokuwa nimeizoea, nimekutana na vitu tofauti sana huku hasa ninapokuwa uwanjani na hata nikiwa nje ya uwanja kuna vitu vizuri ambavyo sikuwahi kuvipata, hivyo nazidi kujifunza kila kukicha.
CHAMPIONI: Changamoto zipi unazokutana nazo na kwa namna moja zinakuwa kero kwako?
MSUVA : Changamoto zipo, si unajua huku nipo ugenini! Kuna vitu nilikuwa nimezoea sana nikiwa Bongo, kama lugha yangu ya Kiswahili ambayo ndiyo nilikuwa naitumia kwa asilimia kubwa na mara chache Kingereza nakijuajua kidogo, lakini changamoto kubwa huku wengi wao hawajui kabisa Kingereza, sanasana wanazungumza Kiarabu na Kifaransa tu, hivyo kuna muda inaniwia vingumu sana kwenye mawasiliano hasa kwa lugha hizi mbili ambazo sizijui.
CHAMPIONI: Ukiwa haupo na timu unafanya nini?
MSUVA: Huwa narudi kupumzika kwangu. Nitaenda wapi na sina ninapopajua?
CHAMPIONI : Chakula cha huko kikoje, na wewe unakula nini?
MSUVA: Ni ngumu kutaja chakula chao (maana hakijulikani ukikiona). Mimi nakula zaidi wali lakini huku unapikwa tofauti na tulivyozoea. Huwa nakula pia potatoes (viazi), kuku au samaki. Na asubuhi ni mikate, maziwa na mayai.
CHAMPIONI: Je, hapo kwenye klabu yako kuna mchezaji mwingine yeyote wa huku Afrika Mashariki?
MSUVA: Hakuna mchezaji yeyote kutoka Afrika Mashariki, ila wapo watatu wanatoka Afrika, kama kuna mmoja anatokea Cameroon, wengine Senegal na Gabon.
CHAMPIONI : Ligi ya huko inaanza rasmi lini, na umeshaanza kubaini utofauti?
MSUVA: Ligi inaanza Septemba mwishoni, pia tofauti ya ligi ya huku na Bongo ipo kidogo tu na siyo sana, zaidi ni uendeshwaji wake ndiyo una tofauti kubwa kwani huku hakuna mambo ya ubabaishaji kama ilivyo kwetu ambapo ratiba imekuwa haiishi kupanguliwa-panguliwa.
CHAMPIONI : Wapinzani wakubwa huko ni timu gani kama ukilinganisha na huku zilivyo Simba na Yanga?
MSUVA: Timu yetu ya Difaa El Jadidi na Wydad Casablanca zina upinzani mkubwa kama ilivyo Simba na Yanga, lakini pia zinapokutana Raja Casablanca na Wydad Casablanca, hii ndiyo derby pekee ambayo mashabiki huwa hawalali usingizi wakisikia timu hizi zinakutana.
CHAMPIONI : Huko unacheza nafasi gani?
MSUVA: Tangu kocha wangu ameniona siku ya kwanza aliniambia nicheze namba 10, maana huyu kocha kasema mimi najua sana kufunga, kwa hiyo hawezi kunichezesha pembeni, badala yake kaniweka pale kati ili niwe huru kufanya lolote na wakati wowote ule hasa nikitaka kufumania nyavu.
MAKALA: MUSA MATEJA TANZANIA
Post a Comment