KESI YA MANJI: MKURUGENZI WA TAASISI YA MOYO MUHIMBILI ATOA USHAHIDI

 AliyekuwaMwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji akisubiri kusikiliza kesi inayomkabili.
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKIC), Prof. Mohammed Janabi, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo anachokifahamu kuhusu Yusuf Manji tokea alipofika katika taasisi yake kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.
Prof. Janab ni shahidi wa kwanza upande wa utetezi ambaye ameelezea mambo mbalimbali ya kitaalamu kuhusiana na matibabu waliyompatia Manji kwa kipindi alichofika katika taasisi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.
Shahidi huyo ametoa ushahidi wake katika kesi inayomkabili Yusuf Manji ya dawa za kulevya ambapo kwa upande wa utetezi alikuwa ni wakili Hajra Mungula.
Katika utetezi wake shahidi huyo amesema anamfahamu Manji baada ya kufikishwa katika taasisi hiyo Februari mwaka huu akiwa mwenye matatizo ya moyo na kwamba alipofikishwa hapo alifanyiwa vipimo na jopo la madaktari lililobaini moyo wake ulikuwa na matatizo.
…Kesi ikiwa bado haijaanza kusikilizwa.

Alifafanua kwamba mnamo Julai mwaka huu alirudishwa tena katika taasisi hiyo akiwa na tatizo hilo la moyo na maumivu ya mgongo na kutopata usingizi.
Prof. Janab amesema Manji alivyorudi hapo walimpokea kama mgonjwa aliyetibiwa nje ya nchi na ripoti ilionyesha ametibiwa Florida, Marekani.
Alipoulizwa na Wakili Mungula kama mgonjwa wa matatizo hayo ya moyo anaweza kutumia dawa za kulevya, Prof. Janab alijibu kwamba mtu wa namna hiyo huwa haruhusiwi kufanya baadhi ya mambo ikiwemo kuvuta sigara, kutumia Heroine na hivyo kama akitumia athari zake ni kwamba mirija ya moyo inaweza kuziba na baada ya hapo anaweza kufanyiwa upasuaji mkubwa.
Aliongeza kuwa katika awamu ya pili ya Manji kurudi hospitalini hapo walimsaidia kumtibu maumivu aliyokuwa nayo kwa kumpa Drip ya Paracetamol’s na sindano.
Kwa upande wa serikali wakili alikuwa ni Timony Vitalis na kesi imeahirishwa hadi kesho Agosti 31 mwaka huu kwa ajili ya kuendelea na mashahidi wengine.
NA DENIS MTIMA/GPL

No comments

Powered by Blogger.