Tambwe: Kwa mziki huu Yanga…

Straika wa timu hiyo, Amissi Tambwe.
SIKU chache baada ya Yanga kumtambulisha Ibrahimu Ajibu aliyetokea Simba, straika wa timu hiyo, Amissi Tambwe amesema kwa usajili walioufanya hadi sasa, anamuonea huruma huruma Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe.
Ajibu amesajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili na kukabidhiwa jezi namba 10 atakayoitumia katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tambwe ambaye ni raia wa Burundi aliliambia Championi Jumamosi kuwa, usajili huo wa Ajibu unaifanya Yanga kuwa na kikosi bora cha ushindani hivyo anamuonea huruma Hans Poppe msimu ujao.
“Ujio wa Ajibu unatufanya tuwe na kikosi bora msimu ujao hasa katika ushambuliaji na naamini tutakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kufunga, hapa namuone huruma Hans Poppe kwani tutafunga sana,” alisema Tambwe.
Licha ya Ajibu, wachezaji wengine waliosajiliwa na Yanga ni kipa Youthe Rostand kutoka African Lyon, Pius Buswita (Mbao FC), Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (Taifa Jang’ombe), Gadiel Michael (Azam FC) na Raphael Daud kutoka Mbeya City.
Wakati anasajiliwa na Yanga akitokea Simba, Tambwe alionekana ameshuka kiwango lakini akawa mfungaji mzuri huku Hans Poppe akisema wakati wanamuacha kikosini hakuwa na makali.
Hata hivyo, Hans Poppe alipotafutwa kuzungumzia kauli hiyo ya Tambwe alisema: “Namtakia kila la kheri lakini namuomba ajue kuwa siwezi kupata presha kwa ajili yake.”

No comments

Powered by Blogger.