Bingwa baiskeli chali, vidume vyaweka rekodi mpya Majimaji Selebuka

  Sehemu ya waendesha baiskeli wa 100 km kutoka wilayani Mbinga kwenda wilayani Songea wakichuana kuisaka nafasi ya kwenda Afrika Kusini kupata mafunzo ya kimataifa ya mchezo huo.
Bingwa wa mbio za baiskeli za 100km, Maulid Amani kutoka Dar es Salaam (Fulani nyeupe/nyeusi) katika mchuano mkali na Hangaya Naftali Sanga wa Mbeya aliyeshika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Tamasha la Majimaji Selebuka

 Washindi katika kategoria mbalimbali, wakiwa katika picha ya pamoja na waratibu wa Tamasha la Majimaji Selebuka
 Mbunge wa Wilaya ya Songea, Leonidas Gama akimkabidhi  tuzo ya bingwa wa mbio za baiskeli za 100 km, Maulid Aman wa Dar es Salaam.
1    Mwakilishi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (Open), akipokea tuzo kutoka kwa Mbunge wa Songea, Leonidas Gama baada ya chuo hicho kuibuka kinara katika maonyesho ya biashara, kategoria ya  Elimu na Huduma kwa Umma.

KINARA wa mbio za baiskeli za 100 km mwaka jana kwenye mashindano ya mchezo huo wa Tamasha la Majimaji Selebuka, Salum Miraj ameangukia pua katika kuitetea nafasi yake kwa kuishia nafasi ya nane safari hii na mbaya zaidi rekodi yake ikipitwa na vidume viwili kwa mpigo.
Katika tamasha la mwaka huu lililoanza kutimua vumbi Julai 23 na kuhitimishwa Jumapili ya Julai 30, mwaka huu ilishuhudia Miraj akiachia nafasi yake kutwaliwa na Maulid Amani wa Dar es Salaam pia.
Hata hivyo ishu ni kwamba licha ya kupigwa chini, pia rekodi yake ya kumaliza katika muda wa 3:10: 17 ikifutwa rasmi na videmu wa kazi, Aman aliyetumia muda wa 3:09:43 pamoja na mshindi wa pili, Hagaya Naftali Sanga muda 3:09:47 wa Mbeya.
Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Elias Zawadi Tala kutoka Mbeya aliyetumia muda wa 3:41, huku mshindi wa tatu katika mbio za mwaka jana, Ipiyana Julias Mbogela mwaka huu akiburuzwa mpaka nafasi ya nne akitumia muda wa 3:30:07.
Katika tamasha hilo ambalo mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Songea, Leonidas Gama jumla ya wapiga pedali 16 walishiriki lakini waliofanikiwa kumaliza mbio ni 13, huku watatu wakishindwa kwa sababu kadha wa kadha.
Watatu kukwea pipa Sauz
Aidha licha ya tuzo za fedha taslim kwa washindi wa kwanza mpaka wa 10, pia washindi watatu wamejihakikishia nafasi ya kwenda Afrika Kusini kwenda kupata mafunzo ya kimataifa ya mchezo huo kwa kugharimikiwa kila kitu na Kampuni ya Tanzania Mwandi na Asasi ya Somi.
NMB, Open wang’ara kwa tuzo
Katika tuzo nyingine za maonyesho ya kibiashara na ujasiriamali, Benki ya NMB ilifanikiwa kuibuka kinara katika kategoria ya Wafanyabiashara na Taasisi za Fedha kwa kuwapiku Mbinga Cofee (wazalishaji wa kahawa) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizoshika nafasi ya pili na tatu.
Nacho Chuo Huria cha Tanzania (Open University) kiliibuka kinara katika kategoria ya Elimu na Huduma kwa Umma kwa kuwapiku vinara wa mwaka jana, Consenuth waliotelemka nafasi moja huku Jeshi la Polisi Songea likishika nafasi ya tatu.
Kwenye kategoria ya Wajasiriamalia wadogowadogo, bingwa alikuwa Kampuni ya Uzalishaji Gypsum inayotengenzwa kwa malighafi za mkoani Ruvuma, wakifuatiwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tecno na Kikundi cha Usindikaji Mihogo kikishika nafasi ya tatu kwa bidhaa mbalimbali zitokanazo na zao la mhogo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tamasha la Majimaji Selebuka, Dr Damas Daniel Ndumbaro, tayari mikakati kuelekea tamasha la awamu ya nne mwakani iko wazi na inatarajiwa kuanza Julai 14-21, mwakani.

No comments

Powered by Blogger.