Kuelekea ubingwa wa Ligi kuu Tanzania Bara, Prof. Jay atoa ushauri kwa Klabu ya Simba

      Professor Jay akiwa kwenye moja ya mechi za Simba uwanja wa Taifa,Dar es salaam

 Rapa mkongwe nchini Tanzania na Mbunge wa Mikumi kupitia tiketi ya CHADEMA, Mh Joseph Haule maarufu kwa jina la ‘Professa Jay’ ameitaka timu yake ya Simba kuweka nguvu zaidi katika fainali ya Kombe la Shirikisho kuliko Ligi Kuu.
Simba ambayo ipo nafasi ya pili kwa pointi 65 wakiwa wametofautiana na Yanga kwa tofauti ya Magoli wote wakiwa na alama sawa huku Wekundu wa Msimbazi wakiwa wamebakiwa na mchezo mmoja na Wanajangwani wakiwa na mechi mbili mkononi.
Profesa Jay licha ya kuiombea timu yake hiyo ichukue ubingwa wa Ligi Kuu, lakini alisema Simba ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa bila wasiwasi wa Kombe la Shirikisho watakapocheza fainali yao dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Mei 28 kuliko ubingwa wa Ligi.
Nguli huyo wa Hip Hop  amesema ubingwa wa Ligi Kuu kwa Simba utatagemeana na mechi za Yanga kama watashinda mechi moja kati ya mbili zilizosalia basi Simba hawatakuwa na chao hata wakishinda mchezo wao wa mwisho hivyo ni vyema zaidi kujipanga kwa fainali ya FA.
“Furaha yangu ni kuona Simba inachukua ubingwa wa Ligi Kuu  Tanzania bara na ubingwa wa Shirikisho kutokana na ubora wa kikosi cha timu yetu hivyo tutashinda mechi zilizobaki na kutwaa ubingwa japo imani yangu kubwa zaidi ipo kwenye Kombe la Shirikisho“,Alisema Professor Jay.
Akizungumzia fainali ya Kombe la Shirikisho itakayochezwa kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma msanii huyo alilipongeza Shirikisho la Soka nchini {TFF} kwa kuipeleka fainali hiyo Makao makuu ya nchi kwani hata yeye na wabunge wengine watapata uhondo wa kushuhudia fainali hiyo.
Chanzo:Mwanaspoti

No comments

Powered by Blogger.