Video: Mjane Amwaga Machozi Mbele ya Rais Magufuli Akidai Kudhulumiwa Mirathi

DAR ES SALAAM: Mjane mmoja (kwenye picha kushoto), mkazi wa Mkoa wa Tanga ameibuka kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na kumwaga machozi mbele ya Rais John Magufuli wakati akitoa malalamiko yake kuhusu kudhulumiwa kwa haki yake ya mirathi baada ya kifo cha mumewe.

Akilia kwa uchungu, mjane huyo amesema kuwa, kesi yake ilitolewa hukumu ambapo nakala ya hukumu aliyopewa yeye ni tofauti na aliyopewa mdaiwa.

Aidha mama huyo alienda mbali zaidi na kusema kuwa malalamiko yake ameshayapeleka kwa DPP, AG, IGP, Waziri wa Sheria, Dkt Mwakyembe na sehemu mbalimbali ambazo aliona zitamsaidia lakini hakuna lolote mpaka sasa.

Mama huyo alienda mbali zaidi na kueleza kuwa imefikia wakati anatumiwa ujumbe wa vitisho vya kuuawa ambapo ujumbe huo aliupeleka polisi na kumtumia Rais Magufuli ili aone namna ambavyo anatishiwa maisha.

“Mheshimiwa rais mimi ni mjane, kuna watu wamefanya mbinu za kunidhulumu mali zangu ambazo nilitafuta na mume wangu, wamevuruga wosia wa mirathi na hata niliposhtaki sikutendewa haki kwani kuna mawakili wamehusika katika kutengeneza mbinu ili nidhulumiwe.

“Hakimu aliyesimamia kesi hiyo ametoa nakala tofauti ya huku ya kesi hiyo, kwangu na kwa mdaiwa.

“Jambo hili DPP, AG, IGP na Waziri Mwkyembe wanafahamu.

“Imefikia wakati ninatumiwa ujumbe wa kuuawa kwenye simu, au kwa kuwa watu hao wanapesa za kuuza madawa ya kulevya? Ninawajua kuwa wanafanya hizo biashara za drugs (madawa ya kulevya) hata picha za ushahidi ninazo,” alisema mama huyo huku akilia kwa uchungu.

“Ninakuomba mheshimiwa rais unisaidie nipate haki yangu, nimeteseka vya kutosha, nina nyaraka zote za ndoa kutoka BAKWATA, Wizara ya Mambo ya Nje ambayo nilipewa kwenye Ubalozi wa Kenya,” alisema mama huyo.

Kwa upande wake, Rais Magufuli alimsimamisha Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu ambaye alikiri kuifahamu kesi hiyo na kuelekeza kuwa inashughulikiwa na mahakama ya wilaya jijini Tanga.

Aidha Rais Magufuli amewaagiza DPP na AG kuhakikisha wanaishughulikia kesi hiyo ili mama huyo aweze kupata haki yake haraka iwezekanavyo kwani suala hilo liko ndani ya uwezo wao.

Kutokana na kutishiwa maisha, Rais Magufuli ameagiza Jeshi la Polisi wampe ulinzi mjane huyo mpaka atakapopata haki yake.

MJANE ALIVYOMWAGA MACHOZI MBELE YA RAIS MAGUFULI AKIDAI KUDHULUMIWA MIRATHI

No comments

Powered by Blogger.