Kauli ya Rais Magufuli Baada Ya CCM Kushinda Kwa Kishindo Uchaguzi Mdogo wa Marudio
Mwenyekiti
wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli amesema ushindi wa CCM wa ubunge na
madiwani katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika juzi nchini ni ishara ya
ushindi wa chama chake katika uchaguzi ujao kutokana na wananchi
kuonesha imani kwake na serikali yake.
Rais
Magufuli aliyasema hayo kwa waandishi wa habari muda mfupi kabla ya
kumpokea Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan aliyefika Ikulu, Dar es
Salaam jana akiwa kwenye ziara yake ya siku mbili nchini.
Rais
Magufuli alisema ushindi huo ni kipimo cha utendaji wake kwa wananchi
na hivyo umemuongezea ari ya kuwatumikia wananchi kwa moyo wake bila ya
kujali changamoto mbalimbali zilizopo.
“CCM
Oyee! Mnaonaje ushindi wa CCM? Hii inadhihirisha ni namna gani wananchi
walivyo na imani na mimi na serikali yangu. Tumeshinda ushindi wa
kishindo katika kata na Jimbo, wenyewe mmeshuhudia namna tulivyowapiga.
Au mnasemaje?” Rais Magufuli aliwaambia waandishi wa habari na kisha
akawashukuru na kuelekea eneo lake maalumu akimsubiria Rais wa Uturuki
kwa ajili ya kumpokea.
CCM
mbali ya kushinda kiti cha ubunge cha Dimani visiwani Zanzibar,
imeshinda kata 18 kati ya kata 20 zilizofanya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani
juzi kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kufa kwa waliokuwa
wakishikilia nyadhifa hizo na kufutwa kwa matokeo kwa amri ya mahakama.
Kata
ambazo CCM imeshinda ni Nyarenanyuki (Arumeru, Arusha), Isegehe
(Kahama, Shinyanga), Nkome (Geita), Kiwanja cha Ndege (Manispaa
Morogoro), Lembeni (Mwanga, Kilimanjaro), Ihumwa (Dodoma), Matevez
(Meru, Arusha), Kimwani (Muleba, Kagera), Igombavanu (Iringa), Kijichi
(Mbagala, Dar es Salaam), Ng’hambi (Dodoma), Kinampundu (Singida),
Kasansa (Katavi), Malya na Kahumulo (Mwanza), Mkoma (Mara), Misugusugu
(Kibaha, Pwani).
Aidha, CCM imeshindwa katika Kata ya Duru mkoani Manyara, ambako mgombea wa Chadema, Ali Shaaban ameibuka mshindi.
Post a Comment