Mfungwa Atoroka kwenye chumba cha mtihani wa Kidato cha nne

Watahiniwa wakaguliwa kuingia katika chumba cha mtihani wa KCPE katika gereza ya Nakuru GK Novemba 1, 2016.
MFUNGWA aliyekuwa mmoja wa watahiniwa wa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) katika gereza la Naivasha aliingiwa na uoga dakika za mwisho akatoroka na kukataa kuingia katika chumba cha mitihani
Mfungwa huyo aliyekuwa miongoni mwa wengine 55 waliosajiliwa kufanya mtihani huo alibadili azimio lake la kielimu muda mfupi kabla ya mtihani kuanza.
Walinzi wa gereza hilo walimtafuta katika kila pembe walimodhani amejificha lakini hawakumpata.
Afisa wa Hali Njema ya wafungwa Bw Moses Kodec alisema: “Hatuelewi kwa nini alibadili nia yake, lakini wafungwa wenzake wamejitayarisha vya kutosha na tunatarajia kuwa watapita.”
Katika gereza hilo, mtahiniwa mwenye umri mkubwa zaidi, Stephen Muira Mwangi aliye na umri wa miaka 64 alionekana kufurahia sana mtihani. Alisema alilenga kupata alama 300 na zaidi.
Mfungwa mwingine ambaye alihukumiwa kunyongwa lakini hukumu yake ikapunguzwa kuwa kifungo cha maisha Samson Wanjala pia alifurahia sana kufanya mtihani wa kitaifa kwa mara ya kwanza.
Alikuwa akilenga kupata zaidi ya alama 400 ili kujiunga na shule ya upili, ndani ya jela hiyo.
Hapakuwa na changamoto wakati mtihani ulipoanza huku maafisa wa polisi wakionekana kudumisha usalama eneo la mtihani.
Maafisa wakuu wa elimu wakiongozwa na Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i waliweka historia kwa kusimamia usambazaji wa karatasi za mitihani katika maeneo tofauti nchini.
Dkt Matiang’i aliwasili katika Kaunti ya Vihiga saa kumi na moja unusu alfajiri akashuhudia jinsi walimu wakuu walivyofungua makasha ya mitihani katika afisi za kaunti ndogo ya Emuhaya zilizo Luanda.
Baadaye alielekea katika vituo tofauti vya mitihani ambapo alichunguza jinsi mitihani ilikuwa ikisimamiwa.
“Wizara itahakikisha mitihani inaendelea bila matatizo hadi itakapokamilika Alhamisi,” akasema.
Katika Kaunti za Homa Bay, Kericho na Kakamega, hapakuwa na matukio ya kipekee kwani mitihani iliendelea bila matatizo yoyote.
Wafungwa 12 katika Kaunti ya Meru walifanya mtihani huo. Wakati huo huo mwanafunzi katika kaunti hiyo alilazimika kufanya mtihani katika Hospitali ya Rufaa ya Meru alikolazwa.
Wanajeshi wa KDF walipewa jukumu la kusindikiza msafara wa mitihani iliyosafirishwa na polisi katika eneo la Diff, Kaunti ya Wajir ambako kumekuwa na mashambulio ya kigaidi miezi iliyopita.
“Huu ni mtuhani wenye ulinzi mkali zaidi ambao nimewahi kuona,” Naibu Kamishna wa kaunti hiyo Felix Kisalu alisema.
Katika Kaunti ya Marsabit, ilisemekana walimu wakuu walilala viungani mwa makao makuu ya kaunti ndogo ili wanafunzi wao waanze mitihani saa mbili kamili kama ilivyoamriwa na serikali.
Hii ni tofauti na miaka iliyopita ambapo mitihani ilikuwa ikianza kuchelewa katika maeneo ya mbali. 
credit edwinmoshi.blog

No comments

Powered by Blogger.