Waziri Mkuu Atoa Mwezi Mmoja Kwa Watumishi Waliohamishiwa Kibiti Kuripoti Kituoni

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa mwezi mmoja kwa watumishi waliohamishiwa wilaya mpya ya Kibiti mkoani Pwani kuripoti katika kituo chao cha kazi na watakaoshindwa kutekeleza watakuwa wamejifukuzisha kazi. 
 
Amesema mtumishi yeyote aliyehamishiwa wilaya hiyo ambaye anaishi nje ya Kibiti anatakiwa arudi na kuishi kwenye makao makuu ya wilaya na si vinginevyo. 
 
"Tayari nimemuagiza ndugu Zuberi Samatabu Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani kuhakikisha anasimamia watumishi wote wa wilaya hiyo wanaoishi nje ya wilaya hiyo waishi Kibiti na si Ikwiriri," amesema. 
 
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu ilifuatia taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Alvera Ndabagoye ambaye alimueleza Waziri Mkuu kuwa ni watumishi wanane pekee kati ya 74 waliopangiwa kufanya kazi kwenye wilaya hiyo wameripoti katika kituo cha kazi 
 
 Ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa nyumba za watumishi amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo kuzungumza na watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii kwenda wilayani huko kuwekeza katika miradi ya ujenzi wa nyumba za watumishi. 
 
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana Jumatano, Septemba 28, 2016 wakati akizungumza na watumishi wa wilaya hiyo katika ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo,utendaji wa serikali na kutoa msimamo wa serikali kuhusu utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku 
 
Wakati huo huo Waziri Mkuu amewataka madiwani wa halmashauri hiyo wawe wakali katika kusimamia miradi ya maendeleo na kuacha tabia ya kuomba omba kwa wakuu wa idara ili kuepuka kujishushia hadhi zao na kupelekea kuhujumiwa kwa miradi mbalimbali ya jamii 
Aidha aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kutengeneza mazingira ya kukaribisha wawekezaji na wahakikishe kwamba uwekezaji utakaofanyika hausababishi migogoro ya ardhi kwa wananchi. 
 
Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi kuhakikisha wanapeleka watoto shule kwa maana Serikali imebeba mzigo wote wa gharama za ada na uendeshaji wa shule hizo. 
 
Alisisitiza kuwa njia pekee na ya haraka kuondoa umaskini ni kusomesha watoto Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameagiza halmashauri zote nchini kutumia mfumo wa kieletroniki katika ukasanyaji wa mapoto ili kuziba mianya ya uvujaji mapato haswa ya maliasili.

No comments

Powered by Blogger.