Rais Magufuli Aridhia Kusaini Miswada Mitano Kuwa Sheria za Nchi
Na Eleuteri Mangi-Maelezo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameridhia na kusaini Miswada mitano
kutumika kama Sheria kamili za nchi.
Hayo yamesemwa na Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai mara baada ya kufungua
Mkutano wa nne wa Bunge la 11 leo mjini Dodoma.
Miswada iliyoidhinishwa na Rais ni
pamoja Sheria ya Fedha na Matumizi ya mwaka 2016, Sheria ya Fedha namba 2
ya mwaka 2016, Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya mwaka
2016, Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbambali namba 2 na 4 ya mwaka
2016 na Sheria ya Marekebisho ya Ununuzi ya Umma namba 5 ya mwaka 2016.
Aidha, Mhe. Spika amewakumbusha
Wabunge kusoma na kuelewa kila kinachokuja Bungeni ili waweze kutekeleza
majukumu yao ya kibunge ipasavyo kwa niaba ya wananchi waliowatuma
kufanya kazi hiyo ili kuwaletea maendeleo.
Wabunge wametakiwa kutekeleza majukumu
hayo ya uwakilishi wa wananchi ili waweze kujadili masuala mbalimbali
kwa kuzingatia haki, ustahimilivu, busara, hekima na kutumia lugha ya
staha katika mijadala ya Bunge.
Vile vile Mhe. Spika amempongeza Naibu
Spika Dkt. Tulia Akson kuongoza vema mkutano wa tatu wa Bunge ulioanza
Aprili 19 na kumalizika Juni 30 mwaka huu kwa kushirikiana na wenyeviti
wa Bunge Andrew Chenge, Mussa A. Zungu na Najima Giga.
Katika hatua nyingine Mhe. Spika
amemshukuru Rais Dkt. Magufuli, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Watanzania wote walimuombea alipokuwa kwenye matibabu nje
ya nchi pamoja na Madaktari waliomhudumia akiwa kwenye matibabu na
kumshukuru Mungu kwa kumwonesha upendo alipokuwa kwenye mapito ya
kuugua.
Katika mkutano huo wa Bunge yameulizwa
maswali 14 ambayo yalielekezwa kwenye Wizara mbalimbali na kujibiwa kwa
llengo la kutolea ufafanuzi masuala yanayotekelezwa kwa Serikali.
Post a Comment