Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni Aagiza Magari yanayokamatwa yakisafirisha wahamiaji haramu yataifishwe
Serikali
imeiagiza Idara ya Uhamiaji kuhakikisha inasimamia sheria kwa
kuyakamata na kuyataifisha magari yote yanayotumika kusafirisha
wahamiaji haramu kutoka nje ya nchi.
Pia,
serikali imewaonya wanaojihusisha na mtandao wa kusafirisha wahamiaji
haramu kuacha mara moja na kutafuta kazi nyingine za kufanya kwani
serikali iko makini kudhibiti wahamiaji haramu.
Agizo
hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf
Masauni, alipotembelea mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Namanga
mwishoni mwa wiki, ili kujionea changamoto zilizopo mpakani na kuelewa
hali halisi.
Masauni
aliwatahadharisha watumishi wa Idara hiyo kuwa endapo gari litakamatwa
katika eneo lolote nchini likiwa na wahamiaji haramu kupitia mpaka huo,
watakuwa wameidanganya Serikali na kuidhihirishia kuwa majukumu yao
yatakuwa yamewashinda.
Alisema
pamoja na kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na idara hiyo ya
uhamiaji Namanga kudhibiti wahamiaji haramu, bado zipo njia za panya
zinazotumiwa na wahamiaji hao mmoja mmoja kwa kushirikiana na Watanzania
wachache wanaofanya kazi ya kuwavusha kwa kulipwa ujira kinyume cha
sheria.
Aliitaka
idara hiyo kutumia vitendea kazi vichache ilivyonavyo pamoja na
waumishi wachache waliopo ili kudhibiti mianya inayotumiwa na wahamiaji
hao. Pia, aliagiza doria za mara kwa mara na kuimarisha ukaguzi ndani ya
magari ili kubaini wahamiaji haramu.
Alisema
idara hiyo inafanya kazi kwenye mazingira magumu kutokana na uhaba wa
vitendea kazi, ukubwa wa eneo la mpaka hivyo akatoa wito kwa wananchi
kusaidia kuwafichua wahamiaji haramu.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alisema idara hiyo
inakabiliwa na changamoto zilizopo mpakani hapo kutokana na ukubwa wa
eneo la mpaka hivyo inashindwa kudhibiti eneo hilo kikamilifu.
Awali,
Mkuu wa idara hiyo katika eneo hilo la Namanga, Abdalah Katimba,
alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo upungufu wa
watumishi na vitendea kazi.
Post a Comment