Msongamano kupima mizigo bandarini kumalizika mwezi huu

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amesema msongamano wa abiria wanaoenda Zanzibar wakati wa kupima mizigo kwenye bandari ya Dar es Salaam utakwisha mwishoni mwa mwezi huu baada ya kukamilika kwa matengenezo ya mashine ya kukagua mizigo iliyoharibika.

Profesa Mbarawa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea eneo la bandari hiyo kwa lengo la kuangalia usalama wa bandari kwa wananchi wanaosafiri kwenda Zanzibar.

Alisema mashine moja ya kukagua mizigo iliharibika tangu Machi mwaka huu na kubaki moja ambayo inafanya kazi na hivyo kusababisha foleni kubwa wakati wa ukaguzi wa mizigo.

“Tayari vifaa vilishaingia na matengenezo yanaendelea na mwisho wa mwezi huu itakuwa imekamilika na zote zitafanya kazi na msongamano utakuwa umekwisha,” alisema.

Aidha, alisema hadi Desemba mwaka huu watakuwa wamefunga kamera katika eneo lote la bandari ili kuangalia wanaoingia kwa usalama wa bandari na wasafiri wanaotumia bandari hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Karim Mataka, alisema wapo kwenye mchakato wa manunuzi kwa ajili ya kufunga kamera hizo.

Aidha, aliwashauri wasafiri wanaotumia bandari hiyo kubeba mizigo michache ili kutunza miundombinu, kwa sababu imeonekana kwamba mashine ya kukagua mizigo imeharibika kutokana na kukwanguliwa na mizigo mikubwa.

No comments

Powered by Blogger.