MO DEWJI; NI MAPENZI TU NA SIMBA, BILIONI 20 NINGEWEZA KUNUNUA KLABU URENO AU KWINGINE ULAYA
Na Saleh Ally
MFANYABIASHARA
bilionea kijana Mohammed Dewji maarufu kama Mo, ametangaza kuwekeza
katika Klabu ya Simba kwa kutoa Sh bilioni 20 ili amiliki hisa kwa
asilimia 51, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki
na wanachama wa Simba.
Lakini
limekuwa gumzo hata kwa wapenda michezo wengi kuhusiana na namna
ambavyo suala hilo linakwenda, kwamba je, Simba wanapaswa kuingia kwenye
mabadiliko au la?
Mashabiki
na wanachama wengi wa Simba, wanaonekana wazi wanachotaka ni mabadiliko
na kwa asilimia kubwa wameanza kuushinikiza uongozi wa timu hiyo
kuhakikisha unaingia kwenye mabadiliko hayo kwenda kwenye kampuni na
baadaye mfumo wa hisa uanze kutumika.
Baadhi
ya wanasiasa, nao wameonekana kuunga mkono ingawa wamekuwa na mawazo
tofauti lakini msisitizo kuwa ni wakati mwafaka kwa Simba kuingia kwenye
mabadiliko hayo.
SALEHJEMBE:,
ilifanya juhudi za kumpata Mo Dewji ili kuzungumza naye kuhusiana na
suala hilo ili kujua maoni yake kwa undani zaidi na nia yake hasa.
SALEHJEMBE: Sh bilioni 20 si fedha kidogo, nini hasa kitakufaidisha wewe kama mfanyabiashara kuingiza fedha hizo ndani ya Simba?
Mo:
Niseme ni suala la kujiuliza lakini jibu la kwanza nitakuambia ni
mapenzi yangu kwa Simba. Lakini ninaamini nitakaposhirikiana na
wanachama na mashabiki wa Simba, tutakwenda kwenye mabadiliko na
kuifanya Simba kuwa klabu bora ambayo ina uwezo wa kushindana barani
Afrika na mwisho mafanikio yatapatikana.
SALEHJEMBE: Unaamini kinachosababisha hivi sasa kuyumba kwa Simba ni fedha peke yake?
Mo:
Lazima uwekeze fedha ndiyo ufanikiwe. Lakini lazima uwekeze mfumo kwa
ajili ya kuziendesha kwa mwendo sahihi hizo fedha. Simba haiwezi
kushindana tena na Yanga na Azam FC kwa kuwa haina fedha. Wao wanafanya
mambo mazuri, wanasajili kwa uhakika, kambi bora, huwezi kuwashindanisha
na Simba.
SALEHJEMBE:Umesema
unatoa Sh bilioni 20, halafu unapenda kuweka bond na baada ya hapo
Simba itatumia faida ya hiyo bond kujiendesha. Sasa fedha unayotumia
inakuwa ni ile uliyonunulia, huoni hapo unapata faida mara mbili?
Mo:
Fedha hiyo ni ile ya Simba, bado inaweza kutumika kwenye maendeleo.
Mimi pia ninaweza kuwekeza zaidi. Pia kumbuka fedha hiyo ya Simba
itakuwa salama itakapokuwa kwenye ‘treasury bond’. Usipoiweka kule
italiwa na mwisho itakuwa Simba ndiyo imepoteza.
SALEHJEMBE:
Umepanga kutoa Sh bilioni 20 upate asilimia 51, una uhakika fedha hizo
ni sawa na thamani hiyo kwa Simba ambayo ina majengo, viwanja na hata
thamani ya nembo yake?
Mo:
Nikuambie ukweli, Sh bilioni 20 ni fedha nyingi sana kwa anayeelewa
biashara. Ningeweza kununua benki au ningeweza kununua klabu ya daraja
la pili barani Ulaya, mfano kwa nchi kama Ureno. Lakini mapenzi ndiyo
yamenisukuma kwenda Simba.
SALEHJEMBE: Nirudie kuhusiana na majengo, huoni yana thamani kubwa na huenda ungepaswa kuongeza?
Mo:
Majengo yale pale Msimbazi thamani yake kupitia utafiti wao Simba ni Sh
bilioni 3.5. Wewe utaangalia vingine vinavyobaki ni kiasi gani.
SALEHJEMBE: Kama unaona Simba thamani yake ni chini, vipi utoe fedha nyingi zaidi?
Mo:
Unapotaka kununua biashara kuna mifumo miwili, mmoja ni Valuation to
Earn Ration. Unamuuliza mtu anaingiza kiasi gani kwa mwezi, labda
anasema ni milioni 100. Halafu wewe unamlipa kwa miezi kumi ambayo ni Sh
bilioni moja. Simba imekuwa ikiingiza hasara tu, ningesema niangalie
hilo, huenda ningelipa kidogo sana lakini nia yangu ni kuendeleza na
kuing’oa ilipo. Inatakiwa fedha nyingi zaidi kuliko ilivyo.
SALEHJEMBE: Umesema kuna mifumo miwili?
Mo: Yaa,
mfumo wa pili ni Asset Valuation. Hapa unaangalia thamani ya mali ya
unachotaka kukinunua, kwa Simba ukiangalia hilo bado ni chini sana. Hata
kama ungeangalia ile nembo, nayo haiingizi faida. Mimi Mo naweza kuwa
nauza maji kwa nembo ya Mo lakini hakuna faida kama siuzi, hivyo siwezi
kusema eti lazima niuze kwa fedha ya juu maana mtu ananunua hasara.
SALEHJEMBE:
Uongozi wa Simba ulikubali kwenda kwenye mabadiliko, ilionekana ni
shinikizo la wanachama. Lakini hawakusema wataufanya kwa muda gani, nini
ushauri wako hapa?
Mo: Katika barua yangu niliyowaandikia, nimewaomba angalau mchakato uchukue miezi mitatu ili tuingie na kuanza kazi.
SALEHJEMBE:Ulisema utakuwa tayari kusaidia usajili, vipi utawapa kiasi gani?
Mo:
Pia niliomba kukutana na viongozi na kamati ya utendaji. Usajili
nitasaidia, mimi ni mwanachama wa Simba. Viongozi wengine hapo akiwemo
Aveva, tulishirikiana pamoja kuisaidia Simba kuivua ubingwa Zamalek
ikiwa timu bora Afrika mwaka 2003, hivyo wanajua kazi yangu na
ninavyoweza kushirikiana na wengine. Kuhusu kiasi, inategemea
tutakavyozungumza.
SALEHJEMBE: Umesema kuna viongozi hawataki mabadiliko, kina nani hasa?
Mo:
Nilisema wanaongozwa na Evans (Aveva), lakini wengi tunafahamiana. Tena
ni wachache tu na mmoja nimemwandikia ujumbe kumueleza nashukuru sana
kuona ananipinga na hataki mabadiliko.
SALEHJEMBE: Kama mabadiliko yatafanyika, wewe ukaingia, unafikiri ndiyo kila kitu kwa Simba kwa maana ya mafanikio?
Mo:
Simba ni klabu kubwa sana, nguvu yake ni watu, fedha ni chagizo la
maendeleo. Mfumo bora ni chachu ya kusukuma na kuleta maendeleo.
Nikiingia bado nitaendelea kuwa karibu na mashabiki na wanachama wa
Simba ili tushirikiane kuingia kwenye mabadiliko ili kutafuta mafanikio.
SALEHJEMBE: Mwisho, unaona mafanikio ya matajiri kama Bakhresa upande wa Azam na Manji upande wa Yanga ndiyo yamekuvuta?
Mo: Labda umesahau, mimi nilikuwa Simba mwaka 2003, kipindi hicho wote hawakuwa wameingia kwenye mpira.
SALEHJEMBE: Vipi ni lazima uwe na asilimia 51 yaani majority share holder, shida nini hasa ukiwa chini ya asilimia 50?
Mo:
Nikiwa chini ya asilimia 50 sina changu, kwanza kumbuka ninawekeza
fedha Sh bilioni 20, si kitu kidogo ndugu yangu. Halafu kama nitakuwa
sina uwezo wa uamuzi wa mwisho, itafikia siku mimi nataka fedha tupeleke
kwenye vijana, wengine hawataki na sina nguvu, mambo yakiharibika, watu
wataniuliza mimi. Hivyo ni lazima niwe nina uamuzi wa kufanya mambo
kukimbilia kwenye mabadiliko na mafanikio.
SALEHJEMBE: Shukrani kwa ushirikiano.
Mo: Ahsante, karibuni wakati wowote.
Post a Comment