KITUO CHA WATOTO WACHANGA YATIMA NJOMBE CHAOMBA MSAADA WA MASHINE YA KUFULIA.

Baadhi ya wafanyakazi wa kituo cha kulelea watoto wachanga Yatima na lishe cha
kipengere Mkoani Njombe wakifua nguo za watoto kwa mikono baada ya
mashine walizokuwa wakizitumia kuharibika, Picha na James Festo.

 
Na James Festo, Njombe.

KITUO cha kulelea watoto yatima na lishe cha Kipengere kinachopatikana
wilayani Wanging'ombe Mkoani Njombe ambacho huwahumia watoto wachanga
yatima wenye umri wa miaka 0 hadi mitano kimewaomba wadau kusaidia
kununua na kutengeneza mashine ya kufulia kutokana na zilizokuwapo
kuharibika baada ya kutumika muda mrefu.

Msimamizi wa kituo
hicho ambacho kwa sasa kinawahudumia watoto 51 miongoni mwa 220 ambao
waliwahi kuhudumiwa na kituo hicho, Sister Nivardina Mbifile aliliambia
gazeti hili mwishoni mwa juma kwamba kwa sasa hulazimika kuamka saa
kumi na moja asubuhi kufua nguo za watoto tofauti na hapo kabla.

""tunachangamoto
kubwa sana ya mashine ya kufulia, tulikuwa nazo zimezeeka zimeharibika
sasa tunafua nguo kwa mikono sasa watoto ni wengi tunaamka saa 10 kufua
nguo za watoto hadi jioni tulionao ni wachanga ...hapo mwanzo tulikuwa
na mashine hata wafuaji walikuwa wanapata nafuu...sasa hivi mikono
inachubuka kwa sasa" alisema Sister Mbifile.

Aliongeza kuwa
"mashine hizi mbili zilishawahi kusumbua na tulisubiri wataalamu kutoka
nje ya nchi wakaja kututengenezea zikaendelea kufanya kazi na sasa
hatuwezi kutengeneza tena...na hii moja haina mda mrefu tumeacha
kuitumia kwa sababu ilianza kuleta maneno ya kichina hivyo tunasubiri
wataalamu kutoka nje wakiwahi watakuwa wametusaidia sana ila tunaomba
mwenye uwezo wa kutusaidia atusaidie.

Umoja wa wananchi wa
Njombe Magharibi waishio jijini Dar es salaam UWENDE ni miongoni mwa
waliofika kutoa msaada ya vyakula na mahitaji muhimu kwa watoto yatima
katika kituo hicho wakiongozwa na Pascal Ngilangwa wenye thamani ya
shilingi milioni 1.08 wakizungumza baada ya kuzungumza na wafuaji wa
Nguo za watoto ambao wengi ni wachanga walisema msaada wa mapema
unahitajika.

"kufua kwa mkono nguo za watoto ambao baada ya saa
moja huwa hazitazamiki kama nepi ni jambo linalohitaji moyo tena si
kidogo tunaomba wadau wengine wasaidie kupatikana kwa mashine ya
kufulia... hata viongozi wa serikali wasaidie hadi Rais wangu Magufuli
mimi namlilia aje asaidie kutengeneza mashine au kununua mashine ya
kufulia" alisema Ngilangwa.

Aliongeza kuwa "sisi tumeamua
kujitolea msaada ni jadi yetu tumekuwa tukisaidia kwenye upande wa
elimu, kilimo, afya na mazingira sisi huchangishana na kutoa misaada
hii kila mwaka katika maeneo mbalimbali.

Kulingana na Sister
Mbifile sehemu kubwa ya watoto ambao hulelewa kituoni hapo wamewapoteza
wazazi wao kutokana na ugonjwa wa ukimwi pamoja na matatizo ya uzazi
wakati wanapojifungua na asilimia kubwa ni kutoka wilaya za Makete,
Njombe na Wanging'ombe. Itakumbukwa Mkoa wa Njombe kwa sasa ndio
unaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya virusi vya
Ukimwi kinachofikia asilimia 14.8 kulingana na utafiti wa Tume ya
kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi humu Nchini TACAIDS iliyotolewa mwanzoni mwa
muongo wa pili wa karne ya 21

No comments

Powered by Blogger.