MENEJA WA DIAMOND AHENYESHWA NA HUKUMU
Babu-TaleHamis Taletale ‘Babu Tale’
Boniphace Ngumije, Amani
BAADA ya juzikati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa
hati ya kukamatwa kwa meneja wa Mbongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Hamis
Taletale ‘Babu Tale’ (picha kubwa) kwa kutotii amri ya mahakama iliyomtaka
kumlipa Shehe Hamis Mbonde Sh. Milioni 250 kwa kupatikana na hatia ya kumtapeli
kazi zake za mawaidha, meneja huyo alijikuta akirudishwa kortini hapo huku
akihenyeshwa.
Kesi hiyo ambayo ilisikilizwa kwa zaidi ya miaka miwili na
kutolewa hukumu, Februari, mwaka huu ilionesha kuwa, Kampuni ya Tip Top Connection
ambayo Babu Tale ni mmoja wa wamiliki, ilitoa na kusambaza kwa kuuza DVDs za
mawaidha ya Shehe Mbonde (mojawapo Uzito wa Kifo) bila makubaliano maalum.
Kwa mujibu wa chanzo, Babu Tale alifikishwa mahakamani hapo,
Jumanne iliyopita chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi huku akionekana
kuchoka sana, pengine kwa mawazo au kwa kutolala sawasawa kama binadamu.
Shehe Mbonde
Mbali na hali hiyo, pia Babu Tale siku hiyo alivaa suruali
ya jinZi iliyochanika kwenye magoti. Haikujulikana ni fasheni au kulikuwa na
misukosuko alikotokea. Chini, kwa maana ya miguuni alivaa ndala au kandambili
hali iliyompotezea uhalisia wake.
Afande mmoja aliyekuwa kwenye msafara wa gari lililombeba
Babu Tale, aliliambia Amani kuwa, jamaa huyo
alitokea Mahabusu ya Kituo cha Polisi, Mbezi Kwa Yusuf jijini Dar ambako
alilala kwa siku moja baada ya kukamatwa, Jumatatu jioni, nyumbani kwake, Mbezi
ya Kimara.
Hata hivyo, mahakamani hapo, Babu Tale alikuwa na mawakili
wanne kwa ajili ya kutengua hukumu ya awali ya mahakama kuhusu kutakiwa kulipa
kiasi hicho cha pesa, lakini baada ya shauri hilo kusikilizwa kwa zaidi ya
dakika 45, ilishindikana.
Mawakili wake wakaomba muda wa kwenda kupitia tena shauri
zima mwanzo hadi mwisho jambo lililomsukuma hakimu kuahirisha kesi hiyo mpaka Ijumaa (kesho).
Ilizungumzwa mahakamani hapo kuwa, Babu Tale aliachiwa huru
kwa masharti ya kufika mwenyewe Ijumaa bila kukosa.
Gazeti hili lilimtafuta Babu Tale bila mafanikio yoyote
kwani simu yake ya mkononi haikupatikana hewani baada ya kutoka mahakamani.
Kesi ya msingi ya Babu Tale ilishasikilizwa na hukumu
kutolewa ambapo alitakiwa kulipa fidia hiyo kwa mlalamikaji lakini ikadaiwa
kuwa, meneja huyo hakutii hukumu hiyo.
Post a Comment